Clooney na shirika la Google kuichunguza Sudan kwa Satalite
29 Desemba 2010►Umoja wa mataifa kwa kushirikiana na Google pamoja na shirika la mcheza filamu George Clooney, wataanzisha mradi wa kuwa na setalite inayoangalia kila kinachofanyika nchini Sudan; mnamo siku hizi nchi hiyo inapojiyarisha kwa kura ya maoni.
Kura hiyo ya maoni itakayoamua ikiwa eneo la kusini linajitenga na kuwa taifa huru au la, inatazamiwa kufanyika tarehe kumi na tisa ya mwezi januari mwaka wa 2011.
Fikra hiyo ya kuwepo satelite inayoangalia kila kinachofanyika nchini Sudan, ni yake George Clooney.
Katika mazungumzo na gazeti la Marekani TIMES, mcheza filamu huyo amesema kuwa fikra hiyo imemjia, alipowatembelea wakimbizi nchini Sudan miezi mitatu iliyopita. Amesema kwamba wakati huo alihisi ni lazima kuwepo kile alichokilinganisha na "mapaparazi dhidi ya mauwaji ya kimbari". Akasema kwamba lengo ni kuwaonya, wale wote watakaokuwa na nia ya kuendesha vitendo vya kikatili na mauwaji; wajuwe kwamba dunia nzima inawaangalia.
Bwana George Clooney, amesema kwamba shirika lake "Not on our Watch" litashirikiana na wacheza filamu wengine mashuhuri, kama vile Brad Pitt na Matt Damon, kugharamia miezi sita ya mwanzo ya mradi huo. Lengo likiwa, kwamba hata baada ya kura ya maoni kufanyika na matokeo yake kutangazwa, utekelezaji wake ufanyike pia katika hali ya usalama.
Shirika la Umoja wa mataifa litachangia kwa kukusanya ripoti kutoka mitambo ya satelite, wakati ambako wataalamu wa chuo kikuu cha Havard watahusika na kutafsiri ripoti hizo; ili kujua nini kilichofanyika, nani waliohusika na wapi-
Ripoti zitaweza kusomwa kwenye mtandao wa Internet; huu ukiwa mchango utakaotolewa na shirika la Google.
Baadhi ya wadadisi wanasema kwamba raia wengi wa maeneo ya kusini mwa Sudan watapiga kura ya kutaka sehemu hiyo ijitenge na kuwa taifa huru. Kura hiyo ya maoni ni hatua ya mwisho ya makubaliano ya amani ya mwaka wa 2005, yaliyofikiwa baada ya vita vya zaidi ya miongo mitatu.
Viongozi wakuu wa nchi mbali mbali na wa mashirika ya kimataifa, wamekuwa wakiendesha juhudi za kuwataka wanasiasa wa Sudan kujiepusha na vita vingine.
Jana jumatano alikuwepo mjini Karthoum, mji mkuu wa Sudan, katibu mkuu wa Jumuia ya nchi za kiarabu Bwana Amr Moussa, ambae alikua na mazungumzo na Rais Omar Al-Bashir wa Sudan pamoja na kiongozi wa kusini Salva Kiir.
Baada ya mazungumzo hayo, Bwana Amr Moussa, alisema kwamba alikuwa na matumaini kwamba pande zote mbili, kusini na kaskazini, hakuna anaetaka vita.
Mda mfupi kabla ya hapo, Rais Omar Al-Bashir, alikua amesema kwamba serikali yake iko tayari kusaidia kusini kuwa na taifa huru linaloishi kwa amani.
Hata hivyo kumekuwepo hali ya wasiwasi mkubwa, hasa katika maeneo ya mpakani baina ya kusini na kaskazini, ambapo wafuasi wa vyama vya upinzani, pamoja na raia wazaliwa wa maeneo ya kusini, wanasema kwamba wamekuwa wakitendewa ukatili na idara za polisi, na wengine kushinikizwa kuhamia kusini; hata kabla ya uchaguzi kufanyika.
Makamo rais wa Marekani Bwana Joe Biden, mwishoni mwa wiki iliyopita alimpigia simu mwenzie wa Sudan Ali Osman Taha, kumuelezea wasiwasi wa serikali ya Marekani; kutokana na ripoti za kuwepo tayari vitendo vya unyanyasaji.
Kulingana na ripoti za Umoja wa mataifa, watu wasiopungua miliyoni mbili wameuwawa katika vita vya waasi wa chama cha SPLM na majeshi ya serikali ya Karthoum, vilivyoendelea kwa karibu miaka thelathini. Raia zaidi ya laki tatu waliuwawa pia katika vita baina ya vyama vya waasi vya maeneo ya magharibi mwa Sudan ya Darfur na majeshi ya serikali ya Rais Omar Al-Bashir; ambae anakabiliwa na waraka wa kukamatwa; uliotolewa na Mahakama ya kimataifa ya vitendo vya jinai.
Muandishi: Jean-François Gisimba
Mhariri: Miraji Othman