1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Makubaliano yalegeza msimamo kuhusu makaa ya mawe

14 Novemba 2021

Mkutano wa kilele wa Umoja wa Mataifa kuhusu mabadiliko ya tabianchi, COP26 umefikia makubaliano Jumamosi jioni ya kuongeza juhudi za kukabiliana na athari mbaya kabisa zitokanazo na mzozo wa kimazingira.

https://p.dw.com/p/42y2z
UN-Klimakonferenz COP26 in Glasgow
Picha: Christoph Soeder/dpa/picture alliance

Mkutano wa kilele wa Umoja wa Mataifa kuhusu mabadiliko ya tabianchi, COP26 umefikia makubaliano Jumamosi jioni ya kuongeza juhudi za kukabiliana na athari mbaya kabisa zitokanazo na mzozo wa kimazingira. Mkutano huo umefanyika kwa wiki mbili mjini Glasgow, Scotland.

Makubaliano hayo yalifikiwa baada ya wajumbe wa mkutano huo kulazimika kufanya majadiliano hadi muda wa ziada wakati mataifa yakivutana kuhusiana na hatua za kuyaendeleza malengo ya kuzuia ongezeko la joto ulimwenguni hadi nyuzi joto 1.5.

Soma Zaidi: Ulimwengu wasubiri mkataba wa COP26

Wamekubaliana nini?

Lengo moja kubwa lililokubaliwa kwenye mkutano huo ni mwito kwa mataifa karibu 200 yaliyohudhuria mkutano huo kuongeza kasi ya hatua za kupunguza matumizi ya makaa ya mawe na kuondoa ruzuku ya mafuta.

UN-Klimakonferenz COP26 in Glasgow | Proteste
Kumekuwepo na maandamano kutoka sehemu mbalimbali ya kushinikiza utekelezwaji wa makubaliano kama hayo.Picha: Dominika Zarzycka/NurPhoto/picture alliance

Makubaliano hayo ya Glasgow pia yameyataka mataifa kutekeleza wajibu wao ili kutimiza lengo kubwa zaidi la kuzuia ongezeko la joto duniani hadi nyuzi joto 1.5, katika wakati ambapo kunashuhudiwa ongezeko la kiasi nyuzi joto 1.1, tangu mapinduzi ya viwanda.

Makubaliano hayo aidha yanayataka mataifa tajiri zaidi kuongeza kiwango cha ufadhili kwa mataifa masikini ili kuyawezesha kutekeleza hatua za vita dhidi ya mabadiliko ya tabianchi.

Sikiliza Zaidi: 

Ajenda ya Afrika kwenye COP26 ilifanikiwa?

Hata hivyo, makubaliano ni kama pigo kubwa kwa mataifa masikini zaidi yanayotaka kulipwa fidia kutokana na hasara na uharibifu uliosababishwa na ongezeko la joto duniani, baada ya Marekani na Umoja wa Ulaya ambao ni miongoni mwa wasambazaji wakubwa wa gesi chafu kuukataa mpango wa usaidizi wa kifedha kwa mataifa hayo.

Masuala yapi yalizua mjadala?

Suala kubwa lililosababisha kutoelewana katika hatua za mwisho za mazungumzo hayo lilihusu namna ya kuweka katika maandishi mpango unaokusudiwa wa kuondoa matumizi ya makaa ya mawe – na badala yake kuudhoofisha kwa kutumia maneno ya "kupunguza matumizi ya makaa ya mawe”.

COP26 in Glasgow | Guillermo Lasso, Boris Johnson und Antonio Guterres
Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres(kulia) ameonya kwamba mataifa yanatakiwa kujihimiza yenyewe kupambana na mabadiliko ya hali ya hewa.Picha: Lee Floyd/Avalon/Photoshot/picture alliance

Makaa ya mawe kwa sasa ndio chanzo kikubwa kabisa cha utoaji wa gesi chafu. India iliongoza waliopinga kubadilishwa kwa maandishi hayo katika dakika ya mwisho, ikisema nchi zinazoendelea bado zinahitaji kutumia mafuta. Wajumbe wengi waliyakosoa mabadiliko hayo.

Nini kimezungumzwa baada ya makubaliano hayo?

Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amesema mkutano huo umeshindwa kufikia malengo yake, lakini aliongeza kuwa ulifanikiwa angalau kufungua njia ya kusonga mbele.

"Haitoshi. Tunatakiwa kuongeza kasi katika hatua za kupambana na mabadiliko ya tabianchi na kuyahusisha malengo ya kuzuia ongezeko la joto duniani. Ni wakati wa kujiweka katika hali ya dharura" alisema Guterres kwenye ujumbe wake kwa njia ya video.

Mwanaharakati chipukizi wa mazingira kutoka Sweden Greta Thunberg pia alielezea kutoridhishwa na matokeo ya mkutano huo wa mwaka huu, akiyataja kama maneno matupu yasiyotekelezeka. "Kazi itaendelea nje ya kuta za Glasgow na hatutaka tamaa" aliandika Greta kwenye ukurasa wake wa Twitter.

Mashirika:DW