COVID: Ujerumani yakumbwa na ‘hali ya dharura’
20 Novemba 2021Waziri wa Afya wa Ujerumani Jens Spahn amesema siku ya Ijumaa kwamba hali nchini Ujerumani imezidi kuwa mbaya kuliko wiki iliyopita na kuongeza kuwa taifa linakumbwa na ‘hali ya dharura ya kitaifa'.
Alipoulizwa kuhusu uwezekano wa kutangaza vikwazo vipya kwa kila mtu, alijibu kwa kusema "Tuko katika hali ambapo hatuwezi kusema hilo haliwezekani.”
Matamshi yake yamejiri mnamo wakati baraza kuu la bunge la Ujerumani limeidhinisha masharti mapya kudhibiti COVID, siku moja tu baada ya bunge kupitisha masharti hayo.
Spahn alikuwa akizungumza na waandishi wa habari akiwa pamoja na Lothar Wieler, mkuu wa taasisi ya kupambana na maradhi ya kuambukiza nchini Ujerumani Robert Koch (RKI).
Wieler alielezea kuhusu taswira ya kutatanisha ya hali ya maambukizi ya virusi vya corona, na kusema katika robo ya wilaya zote nchini, kasi ya maambukizi ni watu 500 katika jumla ya 100,000 na kwamba hospitali zinatishiwa kulemewa, hivyo ipo haja kubadilisha hali hiyo. "Hakuna muda wa kupoteza,' amesema Wieler.
Soma: Wimbi la nne la COVID latishia vizuizi vipya Ujerumani
Wieler pia alisisitiza umuhimu wa chanjo. "Chanjo zinafanya kazi vizuri zaidi,” na kuongeza kuwa ipo haja ya kujaza pengo ambalo limeachwa na wale ambao hawajachanjwa.
Hali halisi ya maambukizi Ujerumani ikoje?
Katika wiki mbili zilizopita, idadi ya maambukizi mapya imeongezeka kwa zaidi ya asilimia 60.
Siku ya Ijumaa, Ujerumani ilirekodi maambukizi mapya 52,970, siku moja tu baada ya kurekodi maambukizi mapya ya watu 65,000, hiyo ikiwa idadi ya juu zaidi ya maambukizi kuwahi kurekodiwa Ujerumani tangu janga lianze. Maafisa wa afya wametahadharisha kwamba huenda takwimu hizo zikaongezeka maradufu katika siku chache zijazo.
Soma: Maambukizi ya COVID-19 yaongezeka Ulaya na kuzusha hofu ya wimbi la nne
Uwe Janssens, katibu mkuu wa chama cha wanaowahudumia wagonjwa mahututi Ujerumani ameiambia DW kwamba idadi ya maambukizi "yanatia wasiwasi.”
Ameeleza kwamba wagonjwa wanaouguza magonjwa sugu baada ya kuambukizwa virusi vya corona hushia kulazwa katika vyumba vya wagonjwa mahututi kuchelewa hata kwa siku 15.
"Kwa sasa takriban asilimia 0.8 ya wale wameambukizwa hutibiwa katika vyumba vya wagonjwa mahututi. Na ikiwa kuna kati ya maambukizi 50,000- 60,000 kila siku, unaweza kuhesabu ni watu wangapi wataweza kupata nafasi katika wodi ya wagonjwa mahututi katika siku 7 hadi 12.”
”Hali inazidi kuwa tete zaidi kumudu,” alisisitiza.
Masharti mapya ni yapi?
Kulingana na mpango mpya, ikiwa zaidi ya watu watatu miongoni mwa wakaazi 100,000 wa eneo moja wataambukizwa COVID-19 na kulazwa hospitalini basi masharti ya "2G” yatazingatiwa katika kumbi zote za starehe na burudani. Na kwamba wale ambao wamechanjwa au wamepona baada ya kuugua ndio wataruhusiwa katika sehemu hizo ikiwemo migahawa na mahoteli.
Masharti ya kiwango cha "2G+” yatafuata ikiwa idadi ya wagonjwa wanaolazwa hospitalini itafikia 6 kati ya kila watu 100,000 katika eneo moja. Hiyo itamaanisha hata wale ambao wamechanjwa au walioopona baada ya kuugua, watalazimika kupima tena na kuthibitisha kuwa hawana virusi hivyo. Takwimu hiyo ikiongezeka na kufikia watu tisa basi viwango vya juu vya masharti vitatekelezwa.
Mipango mingine kwa sasa ni kwamba ni sharti kwa wageni na wafanyakazi wote katika vituo vya kuwahudumia wazee kupimwa kila siku, iwe wamepata chanjo au la.
Aidha katika maeneo ya kazi na usafiri wa umma, watu wanatarajiwa kuthibitisha kwamba wanatii masharti ya kiwango cha "3G” na kanuni zake. Yaani uwe umechanjwa, umepona au umepimwa.
Majimbo yote 16 ya Ujerumani pia yanatarajiwa kuanzisha mikakati ya kuhakikisha kinga zaidi, ikiwemo kuzuia watu kuzuru maeneo ya kujumuika kama bustani, kumbi za kitamaduni, maeneo ya michezo na kupiga marufuku unyaji pombe na kufunga vyuo vikuu.
Hata hivyo hatua hizo hazitalazimisha shule kufungwa, vizuizi vya usafiri au chanjo kwa lazima.
Huenda masharti hayo mapya yakaanza kutekelezwa kuanzia wiki ijayo.
Jimbo la Bavaria latangaza vikwazo kwa wasiochanjwa
Mnamo Ijumaa, jimbo la Bavaria lilitangaza kuwa linafunga masoko yote ya Krismasi jimboni humo.
Serikali ya jimbo hilo pia imetangaza vikwazo vya usafiri katika wilaya zake ambako kwa siku saba zilizopita, kasi ya maambukizi imezidi watu 1000 katika jumla ya 100,000.
Mkuu wa jimbo hilo Markus Söder amesema kutakuwa na kile alichokiita aina ya vikwazo kwa wale ambao hawajapata chanjo, kwa kuhakikisha sheria ya "2G” inatekelezwa kote jimboni humo.
Inamaanisha wale ambao hawajachanjwa katika jimbo hilo hawataweza kuzuru saluni, vyuo vikuu au vituo vya elimu kwa watu wazima. Aidha mkusanyiko wa watu hautaruhusiwa na jumla ya watu watano kutoka familia mbili tofauti ndio wataruhusiwa kujumuika pamoja kwa wakati wowote.
Katika matamasha ya kitamaduni na michezo, asilimia 25 ya idadi jumla inayokubalika ya mashabiki ndio wataruhusiwa, na sheria za 2G+ zitazingatiwa.
Katika maduka, idadi ya watu wanaoingia ndani, itadhibitiwa: Mteja mmoja katika eneo la 10 mraba.
Jimbo la Saxony latangaza masharti mapya
Jimbo la mashariki mwa Ujerumani Saxony, limetangaza masharti mapya siku ya Ijumaa. Masharti hayo yataanza kutekelezwa Jumatatu hadi Disemba 12, ili kudhibiti maambukizi ya COVID yanayozidi kuongezeka.
Masoko yote ya Krismasi kufungwa likiwemo soko kubwa la Dresden.
Vilabu, mabaa, kumbi za mazoezi na makavazi au makumbusho pia yatafungwa. Michezo itaruhusiwa kufanyika lakini bila ya mashabiki.
Aidha kutakuwa na marufuku ya kuwa nje usiku kati ya saa nne hadi kumi na mbili asubuhi.
Maafisa wa Afya wasema ongezeko la maambukizi katika jimbo la Saxony huenda ni kutokana na idadi ya chini ya watu ambao wamechanjwa. Ikiwa ina chini ya asilimia 58 ya watu waliochanjwa, jimbo hilo ndilo la nyuma kabisa nchini Ujerumani miongoni mwa watu waliopata chanjo.
(DW)