Cruz na Sanders washinda Kansas na Nebraska
6 Machi 2016Ushindi wa Ted Cruz katika majimbo ya Kansas na Maine unaonekana kuitia nguvu hoja ya wanaompinga Trump, kuwa siye mgombea bora wa Urais kwa tiketi ya chama cha Republican.
Kwa upande wa chama cha Democratic, Hillary Clinton ambaye anaongoza kwa umaarufu ameshinda katika jimbo la Louisiana huku Bernie Sanders ambaye ni seneta wa jimbo la Vermont akishinda uchaguzi wa mchujo wa vyama katika majimbo ya Kansas na Nebraska.
Uchaguzi huo wa mchujo ulifanyika jana katika majimbo matano. Trump na Clinton wameendelea kuongoza katika azma yao ya kushinda uteuzi wa vyama vyao kuelekea katika uchaguzi mkuu utakaofanyika tarehe nane mwezi Novemba.
Trump ameshinda katika majimbo ya Louisiana na Kentucky. Matokeo hayo ya majimbo matano yalikuwa ni ya kuwavunja moyo wagombea wengine wawili wa chama cha Republican Marco Rubio ambaye ni Seneta wa jimbo la Florida na Gavana wa jimbo la Ohio John Kasich, ambao wamekuwa wakishika mkia katika chaguzi zote za majimbo.
Trump bado yuko kileleni
Cruz ambaye ni seneta wa jimbo la Texas amekuwa akijinadi kwa wapiga kura kama mhafidhina halisi kumliko Trump. Cruz amepata uungwaji mkono kutoka kwa baadhi ya vigogo wa Republican na wanaharakati wa kihafidhina.
Baada ya ushindi wake wa majimbo mawili hapo jana, Cruz amewaambia wanahabari kuwa kile kilichoshuhudiwa katika jimbo la Kansas ni ishara ya kubadilika kwa mkondo wa siasa za Republican.
Trump anaongoza katika kujizolea wajumbe wa kutosha, ili kumuwezesha kupata uteuzi wa chama cha Republican kuwa mgombea wao rasmi wa Urais, lakini amekuwa akishambuliwa vikali katika siku za hivi karibuni kutoka kwa vigogo wa chama hicho.
Chaguzi za Jumamosi zinafikisha idadi ya wajumbe kufika 155 kwa jumla. Matokeo ya jimbo la Maine yanampa Cruz wajumbe 12 na Trump wajumbe tisa.
Katika jimbo la Kansas, Cruz alipata wajumbe 24 ilhali Trump alipata wajumbe tisa. Kinyang'anyiro hicho kinazidi kuwa kikali na kusababisha wengine kuachana na azma yao ya kuwa rais.
Ben Carson alijiondoa kutoka kinyang'anyiro cha kugombea urais siku ya Jumamosi baada ya kushindwa vibaya katika chaguzi za mchujo za majimbo mengi.
Tangu kushinda majimbo saba kati ya 11 katika chaguzi zilizojulikana 'Super Tuesday', Trump amekuwa akimulikwa vikali na viongozi wa chama cha Republican ambao wana wasiwasi kuwa atakisababisha chama hicho kushindwa vibaya sana katika uchaguzi mkuu mwezi Novemba.
Vigogo wa Republican wampinga Trump
Miongoni mwa masuala yanayowatia wasiwasi vigogo wa Republican ni msimamo mkali wa Trump dhidi ya wageni nchini Marekani, ambapo ameahidi kujenga ukuta katika mpaka wa kati ya Marekani na Mexico. halikadhalika ameahidi kuwarejesha makwao wahamiaji milioni 11, ambao hawajapata hifadhi na kuwazuia raia wa kigeni waislamu kuingia Marekani.
Mitt Romney aliyegombea urais mwaka 2012 kwa tiketi ya Republican amemtaja Trump kuwa tapeli na bandia anayecheza na akili za wapiga kura huku mgombea urais wa chama hicho mwaka 2008 John McCain ambaye ni seneta wa jimbo la Arizona akisema sera za kigeni za kigeni ni hatari.
Kundi la vigogo wa Republican linalopinga azma ya Trump lina muda mchache kumzuia mfanyabiashara huyo tajiri kushinda tiketi ya Republican.
Kabla ya Jumamosi, Trump alikuwa na wajumbe 319 kati ya 1,237 wanaohitajika kumpa yeye ushindi katika kunyakua ushindi wa kuwa mgombea atakayepeperusha bendera ya chama chake. Mkutano mkuu wa Republican utafanyika mwezi Julai. Cruz ana wajumbe 226.
Mnamo tarehe 15, Machi chaguzi za mchujo wa vyama zitafanyika katika majimbo yenye wajumbe wengi ya Florida, Illinois, Ohio, Missouri na North Carolina. Majimbo hayo matano yana wajumbe 358 kwa jumla.
Mwandishi: Caro Robi/Reuters/afp
Mhariri: Yusra Buwahyid