1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Daktari wa Congo akabidhiwa tuzo ya Sakharov

Mjahida26 Novemba 2014

Tuzo ya Sakharov inayotolewa na Bunge la Ulaya kwaajili ya utetezi wa haki za binaadamu inakabidhiwa kwa daktari wa nchini Congo Dr Denis Mukwege kwa kazi yake ya kuwasaidia maelfu ya waathiriwa wa ubakaji

https://p.dw.com/p/1Dtu7
Daktari Dennis Mukwege
Daktari Dennis MukwegePicha: picture-alliance/dpa

Daktari Mukwege amekabidhiwa tuzo hiyo kutokana na juhudi zake za kuwasaidia wanawake wanaopitia visa vya unyanyasaji wa kingono katika maeneo ya kivita. Mwaka wa 1998 Mukwege aliye na umri wa miaka 59 alianzisha hospitali yake ya Panzi mjini Bukavu nchini Congo na hadi sasa bado anaendeleza juhudi zake za kuwasaidia waathirika wa ubakaji.

Na ndio maana tarehe 21 mwezi Oktoba mwaka 2014, bunge la Ulaya likaamua kumtambua Daktari huyo kwa kumtangaza mshindi wa tuzo hiyo ya Sakharov anayokabidhiwa rasmi hii leo mjini Strasbourg, Ufaransa.

"Tunatarajia kupata suluhu ya kusimamisha ubakaji kutumiwa kama ngao katika vita na wakati mwengine kama mkakati wa kuanzisha vita." Alisema daktari Dennis Mukwege ambaye licha ya kupokea vitisho vya mara kwa mara pamoja na familia yake kushambuliwa, bado ameendelea kuwasaidia wanawake wengi waliobakwa katika maeneo ya migogoro.

Alipoulizwa ni kwa namna gani tuzo hii itakavyoinua kazi zake, Daktari Mukwege alisema tuzo hiyo inampa moyo zaidi ya kuendeleza juhudi zake na kwamba wanahisi kwamba bunge la ulaya limetambua machungu na ugumu unaopitiwa na wanawake katika vita.

Mkurugenzi wa hospitali ya Panzi mjini Bukavu Daktari Dennis Mukwege
Mkurugenzi wa hospitali ya Panzi mjini Bukavu Daktari Dennis MukwegePicha: Stina Berge

Amesema ubakaji una madhara na makovu makubwa katika jamii huku akisisitiza kuwa anaamini siku moja visa kama hivi havitatumiwa kuwadhalilisha wanawake katika maeneo ya vita.

“Ubakaji unaofanywa na makundi ni silaha ya kivita kwenye eneo lenye utajiri wa madini. Silaha rahisi kwelikweli lakini pia inayofanya uharibifu kama bomu,” alisema Daktari Mukwege.

Wahanga wa ubakaji waelezea masaibu waliyoyapitia

Wakati huo huo mmoja wa wahanga waliookolewa na daktari Dennis Mukwege Honorata Kinzete anasema maisha waliokuwa nayo mashariki mwa congo yaliwageuza wanawake kuwa vyombo vinavyoweza kutumiwa kingono wakati wowote na wanaume.

“Nilikuwa mwanamke wa kila mmoja na bado sikuwa wa yeyote. Kila mwanamme aliyetaka kukidhi haja zake za ngono, alikuwa akiangukia kwetu wanawake. Wakati mwengine walikuwa wakipiga kelele: “Chakula! Chakula!” Na mwanzoni tulikuwa tukidhani tunaletewa chakula, lakini haikuwa hivyo. Sisi wanawake ndio tuliokuwa chakula chao,” alisema Honorata Kinzete

Daktari Dennis Mukwege
Daktari Dennis MukwegePicha: Hugues Honore/AFP/Getty Images

Kinzete anasema kutambuliwa kwa masaibu wanayopitia wanawake wakati wa mizozo inawapa matumaini kwamba dunia inatambua hilo na kuwa mstari wa mbele kutaka kuwanasua wanawake katika janga hili.

Amesema kila mtu anapaswa kufahamu kwamba ubakaji unamdhalilisha mwanamke. “Kumbaka mwanamke au mtoto mbele ya kila mtu na kuharibu viungo vyake sio tendo la kingono pekee ni uharibifu mkubwa wa akili na hata mwili”, alisema Kinzete.

Tuzo hii ya Sakharov inayotolewa kwa daktari Dennis Mukwege inatambua michango muhimu katika kutetea haki za binaadamu na kuinua demokrasia duniani kote.

Mwandishi Amina Abubakar/EU

Mhariri Mohammed Abdul-Rahman