1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Dar es Salaam kupambana na biashara ya ngono

31 Oktoba 2018

Mamlaka ya mkoa wa Dar es Salaam nchini Tanzania imeunda kamati nne kwa ajili ya kupambana na biashara za ngono na mapenzi ya jinsia moja, ili kukabiliana na uvunjwaji wa maadili na sheria nchini humo.

https://p.dw.com/p/37RmW
Tanzania Paul Makonda
Picha: E. Boniphace

Paul Makonda mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam ametangaza kamati hizo mapema leo kutokana na kile alichokitaja kushamiri kwa biashara ya ngono, kukithiri kwa madanguro, nyumba za kutengeneza filamu za ngono lakini pia vitendo vya ushoga na usagaji.

Makonda amesema kuwa kwa watengenezaji wa picha za ngono wamekuwa wakiwachukua wanawake bila hiyari yao lakini wengine wamekuwa wakiridhia na kukubaliana malipo jambo alilolitaja ni kinyume cha sheria za taifa hilo.

Kwa mujibu wa sheria nchini Tanzania vitendo vya umalaya na ushoga ni kosa la jinai na kinyume cha utamaduni wa taifa hilo. Nchi nyingi barani Afrika zimekuwa zikipinga vitendo vya mapenzi ya jinsia moja hasa ushoga ispokuwa taifa la Afrika kusini pekee.

Hata hivyo baadhi ya mataifa yalioondelea ambayo ni washirika wakubwa wa maendeleo katika taifa hilo yanaruhusu na kutambua vitendo vya ushoga ni sehemu ya haki za binadamu hivyo hakuna budi kuheshimiwa na kukubaliana nalo. Katika hili makonda anatoa rai kubwa kwa mashirika na mataifa hayo kutoingilia kampeni hiyo alioianzisha kwa kile anachosema hilo ni kinyume cha sheria, taratibu na utamaduni wa mtanzania.

Kamati alizoziunda mkuu huyo wa mkoa ni kamati ya kupambana na ushoga na usagaji, biashara ya ngono, kukabiliana na usambazwaji na utengenezwaji wa picha za ngono pamoja na kamati maalum ya kupambana na masuala ya utapeli.

Kamati zote hizo zimekuwa na mseto wa wataalamu ikiwemo wanasaikolojia, madaktari, viongozi wa dini wataalamu wa masuala ya mawasiliano pamoja na askari.

Mwandishi: Hawa Bihoga Dw Dar es Salaam
Mhariri:Yusuf Saumu