DAVOS: Kansela wa Ujerumani, Angela Merkel, afungua mkutano wa dunia wa kiuchumi, World Economic Forum.
25 Januari 2007Kansela wa Ujerumani, Bibi Angela Merkel, amefungua mkutano wa dunia wa kiuchumi, World Economic Forum, mjini Davos, Uswisi kwa hotuba iliyoeleza mpango wa serikali yake wakati wa kipindi cha urais wake wa Umoja wa Ulaya na kundi la mataifa manane yaliyostawi kiviwanda, G8.
Bibi Angela Merkel amesema serikali yake imepania kuzingatia kauli mbiu „Uhuru zaidi kwa usalama mpya“ wakati wa kipindi chake cha urais wa Umoja wa Ulaya.
Bibi Angela Merkel pia alizungumzia biashara ya kimataifa ambapo aliyakosoa mataifa yanayojitahidi kujikinga na athari za utandawazi.
Bibi Merkel alisema pande zote zinazohusika zinapaswa kuregeza misimamo yao ili kufufua mashauriano ya biashara ya dunia yaliyokwama.
Kansela huyo wa Ujerumani amesema:
"Nina yakini kwamba utaratibu wa utandawazi ni utaratibu wa kurahisisha biashara duniani. Unatoa uhuru zaidi na ni salama. Hii ndio sababu nikauzungumzia kwa niaba ya serikali yangu inayoshikilia urais wa Umoja wa Ulaya ili tuwe na mustakabali mwema barani Ulaya“
Kiasi viongozi elfu mbili na mia tano wa kisiasa na kibiashara wanahudhuria kikao hicho nchini Uswisi.