DAVOS : Merkel aelezea mipango ya Ujerumani
25 Januari 2007Kansela Angela Merkel wa Ujerumani amefunguwa Kikao cha Uchumi Duniani huko Davos nchini Swirtzerland kwa hotuba yenye kuelezea mipango yake wakati huu Ujerumani inaposhikilia wadhifa wa Urais wa Kundi la Mataifa Manane yenye Maendeleo ya Viwanda Duniani na Umoja wa Ulaya.
Merkel amesema anataka nchi yake wakati ikishilia Urais wa Umoja wa Ulaya kwa miezi sita kuendesha shughuli zake chini ya wito wa uhuru zaidi kwa ajili ya usalama mpya.Kuhusu suala muhimu la biashara ya dunia amesema nchi ambazo zinachukuwa hatua za kuhami masoko yao kupambana na athari za utandawazi zinafuata mkodo usio sahihi.Merkel amesema maridhiano zaidi yanahitajika kutoka pande zote ili kufufuwa mazungumzo ya biashara duniani ambayo yamekwama.
Suala la mabadiliko ya tabia nchi linategemewa kuwa suala jengine kuu la sera.
Takriban wanasiasa na viongozi wa biashara 2,500 wanahudhuria kikao cha mwaka huu.