Dhulma za kijinsia zaongeka Kenya
15 Aprili 2020Akizungumza na wanahabari, katibu wa kudumu katika wizara ya Afya daktari Mercy Mwangagi amesema kuwa hospitali nyingi zinapokea waathiriwa wengi wa dhulma za kijinsia wakati huu ambapo taifa linapopambana na ugonjwa wa covid 19. Hayo yanajiri wakati ambapo kisa cha msichana wa miaka 16 aliyetekwa nyara na jirani yake kuripotiwa hivi majuzi.
Msichana huyo anasemekana kudhulumiwa kwa siku nne kabla ya kuokolewa na majirani ambao waliripoti kisa hicho kwenye kituo cha polisi. Mshukiwa alipoulizwa, kwa nini alifanya kitendo hicho alisema kuwa alitaka mwenziwe wakati huu ambapo watu wamewekewa marufuku ya kutembea kuanzia saa moja usiku.
Wizara Afya imeripoti visa 2000 tangu kuripotiwa kwa mgonjwa wa kwanza wa virusi vya Corona. Mercy Mwangangi ni katibu wa Kudumu katika Wizara ya Afya.
Hadi tukienda mitambani, visa hivyo vilikuwa vimeongezeka kwa asilimia 46 kwa mujibu wa baraza la haki la taifa. Asilimia 80 ya visa hivyo ni vya wanawake na wasichana. Kwa upande wake Idara ya Mahakama imesema kuwa visa ambavyo vimeripotiwa vimeongezeka kwa asilimia 35.
Ni changamoto kwa waathiriwa kwani kwa sasa shughuli nyingi kwenye idara ya mahakama zimefungwa, huku kesi zenye uzito zikiendeshwa kupitia mitandao. Jane Anyango ni mwanaharakati wa kutetea haki za Binadamu katika mtaa mkubwa wa mabanda wa Kibra. Anaafikia kuwa visa hivyo vimeongezeka katika kipindi hiki haswa kwa wasichana.
Hata hivyo Anyango anasema kuwa idadi kubwa ya wanaodhulumiwa pia hawaripiti visa hivyo kutokana na uutamduni. Mwanaharakati huyo anawashauri wanaodhulumiwa kuripoti visa hivyo ili wale wenye nia ya kuwanyanyasa wazuiliwe kufanya uhalifu huo. Linet ambalo si jina lake halisi, alipigwa na mumewe na sasa anahofia maisha yake. Kwani licha ya kuripoti, mumewe hajachukuliwa hatua za sheria.
Serikali ya Kenya imeweka mikakati madhubuti ya kukabiliana na ugonjwa wa COVID-19. Lakini mikakati hiyo imekuwa na athari hasi kwa wanawake na wasichana ikiwemo za kudhulumiwa.
Dhulma za kijinsia zimetajwa kuwa na athari kwa wanawake na wasichana ikiwemo majeraha, maradhi ya zinaa pamoja na matatizo ya kisaikolojia. Asilimia 50 ya visa vya dhulma za kijinsia zilizoripotiwa mwaka uliopita, huku wanawake 100 wakiuawa na wapenzi wao nchini Kenya. Dhulma hizo ni kinyume cha sheria katika katiba ya Kenya.
Shisia Wasilwa, Dw, Nairobi