Dhuluma dhidi ya waandishi wa habari Kenya zaongezeka?
5 Machi 2019Visa vya dhuluma dhidi ya waandishi wa habari vimeripotiwa kuongezekana nchini Kenya huku pakiwa na uwezekano wa visa hivi kuongezeka maradufu mwaka huu ikilinganishwa na mwaka jana 2018.
Naibu afisa mkuu mtendaji wa baraza la vyombo vya habari nchini Kenya, Victor Bwire, anasema kati ya mwezi Januari na Februari mwaka huu tayari wamepokea ripoti 18 kutoka maeneo mbali mbali ya nchi na wanahofia huenda visa vya dhuluma dhidi ya waandishi wa habari vikiangozeka ikizingatiwa kuwa walipokea ripoti za dhulma 35 katika kipindi kizima cha mwaka 2018 walipokea ripoti 35.
Bwire ambaye pia ni meneja wa mipango katika baraza hilo anasema miongoni mwa sababu zinazochangia ongezeko la dhulma dhidi ya waandishi wa habari nchini Kenya ni matukio ya kisiasa hasa uchaguzi mkuu, na wa serikali za majimbo ambapo wanahabari wamekuwa mbele katika kufichua sakata mbali mbali za ufisadi katika serikali za kaunti:
Bwire ameendelea kusema "Ni kweli, kumekuwa na tatizo, waandishi wa habari wengi katika kaunti wanatoka katika hizo kaunti ndio kwao nyumbani, sasa ikiwa kwamba wanasiasa ama wafanyibiashara ambao wanajihusisha kupora mali ya umma ni watu ambao mnaishi nao imekuwa maisha ni magumu kwa waandhisi wa habari."
Bwire amesema miongoni mwa maeneo ambayo wamekuwa wakipokea malalamiko ya dhuluma kutoka kwa waandishi wa habari ni Nyandarua, Migori, Homabay, Turkana, Kisumu, Kitui miongoni mwa maeneo mengine.
Mwanaharakati wa kutetea maslahi ya kibinadamu jijini Kisumu Bonface Akach anasema, waandishi wa habari wamekuwa wakijikuta kwenye hali tata wakiwa kazini na polisi wakichangia dhulma hizi: "Mara kwa mara tumeona wakishambuliwa na hata wakati wa kura tulimuona polisi alikuja kwa kichwa ngumu na akarusha kitoa machozi ndani ya gari lao."
Mactilda Mbenywe mwandishi wa habari shirika The Standard jijini Kisumu, ni miongoni mwa waandishi wa habari waliodhulumiwa na wananchi mbali na maafisa wa usalama: "Ilikuwa wakati wa uchaguzi mkuu hapa nchini, wakati ule kuna mambo mengi yalikuwa yanafanyika unapata waandishi wa habari walikuwa wanapigwa na polisi ama wananchi."
Katika orodha ya waandishi wa habari wasio na mipaka, taifa la Kenya linaorodheshwa katika nafasi ya 96 kwa visa vya dhulma kote ulimwenguni.