Dk. Mukwege na Murad washinda Tuzo ya Nobel ya Amani
5 Oktoba 2018
Tangazo la ushindi wa Dk. Mukwege na Murad wa Tuzo ya Nobel limetolewa na mwenyekiti wa kamati ya tuzo hiyo Berit Reiss-Andersen mjini Oslo muda mchache uliopita. Bi Reiss Andersen amesema wote wawili wamekuwa nembo ya mapambano dhidi ya janga la unyanyasaji wa kingono, ambalo limeenea kutoka mzozo mmoja hadi mwingine, kama vuguvugu la MeeToo lilivyodhihirisha.
''Washindi hawa wawili wametoa mchango mkubwa katika kuumulika na kuupinga uhalifu huo wa kivita. Dennis Mukwege ni mtu aliyejitolea maisha yake kuwasaidia wahanga hao. Nadia Murad ni shahidi anayesimulia unyanyasaji, uliofanywa dhidi yake na dhidi ya wengine.'' Amesema Reiss-Andersen.
Mchango katika kuwafichua wahalifu
Mwenyekiti huyo wa kamati ya tuzo ya Nobel, amesema kila mmoja kati ya watu hao, ametoa mchango kwa njia ya kipekee katika kufichua visa vya unyanyasaji wa kingono katika mizozo na vita, na kusaidia kuwatangaza wahusika wa uhalifu huo ili wakawajibishwe kwa matendo yao.
Dk. Mukwege anasifiwa kwa kujitolea maisha yake yote ya utu uzima kuwatibu maelfu ya wahanga wa ubakaji na unyanyasaji mwingine wa kijinsia katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo - hususan eneo la mashariki mwa nchi hiyo, na kuwa sauti ya kuwatetea. Oktoba mwaka 2012, Dk. Mukwege alinusurika jaribio la kumuuwa, ambapo dereva wake alipoteza maisha
Nadia Murad ni mmoja wa wasichana na wanawake wa kiyazidi wanaokadiriwa kufika 3,000, ambao walibakwa na kufanyiwa unyanyasaji wa kila aina na wanamgambo wa kundi linalojiita Dola la Kiislamu, IS, na amejitokeza kwa ujasiri kuzungumzia madhila yaliyomkuta pamoja na wenzake.
Nembo ya umoja wa kimataifa
Kamati ya Tuzo ya Nobel imesema Mukwege na Nadia wamekuwa alama ya umoja wa kitaifa na kimataifa, katika kupambana na unyanyasaji wa kingono katika maeneo ya mizozo.
Washindi waliotangazwa leo wamechaguliwa kutoka orodha ya watu 216 na mashirika 115, ambayo ilikuwa imewasilishwa mbele ya kamati. Orodha hiyo ni ya pili kwa ukubwa kuwahi kupokewa na kamati hiyo.
Mwandishi: Daniel Gakuba/afpe,dpae
Mhariri: Iddi Ssessanga