1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Usalama waimarishwa Kampala kabla ya maandamano yaliyopangwa

23 Julai 2024

Mamlaka nchini Uganda zimeagiza vikosi vya jeshi na polisi kuzingira maeneo ya bunge ili kuyadhibiti maandamono yaliyopangwa kufanywa na vijana katika jiji la Kampala.

https://p.dw.com/p/4id1Q
Maandamano Uganda
Doria kali za usalama katika mji mkuu wa Uganda kabla ya maandamano yaliyopangwaPicha: Badru Katumba/AFP/Getty Images

Katika picha zilizorushwa hewani na kituo cha Televisheni cha NTV cha nchini humo, zimeonesha wanajeshi waliobeba silaha wakizunguka mitaani, kufuatia kile jeshi la polisi ilichoeleza kuwa ni kuwepo na hatia ya vitendo va kijasusi vinavyopangwa kufanywa na vijana wahalifu.

Wabunge wa upinzani Uganda wafungwa jela kabla ya maandamano ya kupinga rushwa

Barabara za kuelekea bungeni zimefungwa, kwa sababu za kiusalama, ambapo wanaoruhusiwa kupita ni maafisa wa utumishi sambamba na wabunge. Huku wafanyabiashara walio na ofisi zao karibu na bunge, wakipata ugumu kufika katika maeneo yao ya kazi.

Vijana nchini Uganda wamepanga kuandamana kuelekea bungeni kupinga kile wanachodai kuwa ni rushwa na ukosefu wa haki za binadamu sambamba na unyanyasaji unaofanywa na serikali ya Rais Yoweri Museveni.