Dortmund na PSG zatinga nusu fainali Ligi ya Mabingwa Ulaya
17 Aprili 2024Dortmund iliizaba Atletico Madrid 4 – 2 na kufuzu kwa jumla ya mabao 5-4, wakati PSG walipambana na kushinda 4-1 dhidi ya Barcelona iliyokuwa na wachezaji 10 uwanjani na hivyo kufuzu kwa jumla ya mabao 6 - 4.
Soma pia: Dortmund na PSV walitoka sare nchini Uholanzi
Julian Brandt aliiweka BVB kifua mbele katika dakika ya 34 na Ian Maatsen akaongeza la pili dakika tano baadae. Lakini Atletico walirejea mchezoni dakika nne baada ya kipindi cha pili kuanza baada ya beki wa Dortmund Mats Hummels kujifunga. Bao la kusawazisha likapatikana dakika ya 64 kupitia Angel Correa, lakini Niklas Füllkrug akairejesha BVB mchezoni katika dakika ya 71 naye Marcel Sabitzer akafunga kazi dakika tatu baadae na ya kuyaweka hai matumaini ya Dortmund katika Ligi ya Mabingwa.
Kocha wa Dortmund Edin Terzic anahisi kuwa timu yake, ambayo ilishinda Ligi ya Mabingwa mwaka wa 1997, sasa imejiandaa vizuri kukabiliana mabingwa hao wa Ufaransa, baada ya Wajerumani hao kupoteza mechi ya ugenini na kutoka sare nyumbani katika hatua ya makundi. Hii ni mara ya kwanza tangu msimu wa 2012-13, wakati walipopoteza fainali dhidi ya Bayern Munich, kwa Dortmund kufika nusu fainali.
Barcelona wasambaratika mbele ya PSG
Nchini Uhispania, Raphinha aliipa Barcelona uongozi katika dakika ya 12, lakini ghafla wakapunguzwa hadi wachezaji kumi wakati beki Ronald Araujo alipooneshwa kadi nyekundu katika dakika ya 29 na Ousmane Dembele akasawazisha kabla ya mapumziko kwa kuifunga klabu yake ya zamani. PSG waliongeza goli la pili kupitia Vitinha, muda mfupi kabla ya kocha wa Barcelona Xavi Hernandez kuoneshwa kadi nyekundu.
Mambo yaliharibika kabisa kwa timu hiyo ya Uhispania wakati Joao Cancelo alipeana penalty na Kylian Mbappe akasukuma shuti wavuni na akafunga bao lake la pili katika dakika za jioni kuhakikisha kuwa PSG wanayapindua matokeo yam kondo wa kwanza. Mbappe amesema baada ya mechi kuwa "ana ndoto ya kushinda Ligi ya Mabingwa akiwa na PSG”
Wakati kocha wa PSG Luis Enrique ambaye aliwahi kuwa mwalimu wa Barcelona alisema baada ya mechi kuwa anajisikia fahari kubwa kwa sababu wachezaji wake walijituma katika ushindi huo, kocha wa Barca Xavi alimlaumu mwamuzi wa mechi. "Nadhani kadi nyekundu aliyoitoa haikuwa lazima, haikuwa ya haki na haikuwa na maana."
Katika mechi za leo, Real Madrid wanakaribishwa nchini Uingereza kukabana koo na Manchester City wakati matokeo ya mechi ya kwanza yakiwa 3 – 3. Nao Bayern Munich wanawaalika Arsenal dimbani Allianz Arena. Mechi ya kwanza ilikamilika kwa sare ya 2 – 2.
afp, dpa, ap, reuters