DRC iko katika tahadhari kutokana na ugonjwa usiojulikana
6 Desemba 2024Waziri wa afya Samuel Roger Kamba amewaambia waandishi wa habari mjini Kinshasa kuwa mamlaka iko macho na kwamba wanafuatilia mlipuko wa ugonjwa huo kwa ukaribu sana.
Waziri huyo amesema jana kuwa wamehesabu miili ya watu 27 katika vituo vya afya waliokufa kutokana na ugonjwa huo.
Ugonjwa huo unasababisha dalili zinazofanana na mafua makali ambazo ni homa, kikohozi na maumivu ya kichwa.
Ugonjwa usiojulikana nchini Kongo umesababisha vifo vya watu kadhaa.
Ugonjwa huo uligunduliwa kwa mara ya kwanza mwishoni mwa mwezi Oktoba, na hadi sasa umeripotiwa zaidi katika eneo la Panzi, takriban kilomita 700 kusini mashariki mwa mji mkuu Kinshasa.
Kamba ameongeza kuwa watu wengine 44 wameripotiwa kufariki pia lakini ameweka bayana kuwa huenda vifo hivyo vimetokana na sababu nyingine.