DRC kujiunga rasmi na Jumuiya ya Afrika Mashariki
29 Machi 2022Taarifa iliyotoleawa na sekretarieti ya jumuiya ya Afrika Mashariki inaeleza kwamba mkutano huo ambao utawajumuisha marais sita wa nchi wanachama wa jumuiya ya Afrika Mashariki, utaoneshwa mubashara kwa njia ya mtandao na utazingatia mapendekezo ya kikao cha 48 cha baraza la mawaziri wa jumuiya hiyo, kilichoketi siku ya tarehe 25 mwezi huu wa Machi. Ajenda kuu ya mkutano wa leo ni kuiidhinisha Congo kuwa mwanachama mpya wa jumuiya ya Afrika Mashariki.
Congo iliomba kujiunga na jumuiya hiyo tangu mwezi Februari mwaka 2021 na mamlaka husika zilikuwa bado zinapitia ombi hilo kwa kuzingatia mkataba wa kuanzishwa kuwa jumuiya ya Afrika Mashariki. Awali katika mkutano wa 18 wa wakuu wa nchi uliofanyika mwaka jana 2021, katibu mkuu wa jumuiya ya Afrika Mashariki Dr. Peter Mathuki alibainisha kuwa mwezi Machi mwaka huu hatua zote za Congo kujiunga na jumuiya hiyo, zitakuwa zimekamilika.
Kikao kilichotangulia cha baraza la mawaziri wa jumuiya hiyo , kimependekeza kwamba wakuu wa nchi katika mkutano wao wa leo, wazingatie ripoti ya timu ya uhakiki kuhusu maombi ya jamhuri ya kidemokrasi ya Congo ya kujiunga na jumuiya hiyo. Katibu mkuu wa umoja wa mataifa Antonio Guterres aliwahi kutoa wito kwa nchi duninai kuimarisha ushirikiano wa kimataifa wa kikanda na hata kiulimwengu, na hivyo jumuiya ya Afrika Mashariki inachukua wigo wa kupanua uanachama wake kutoka nchi sita hadi kufikia saba.Rwanda yafungua tena mpaka na Uganda, miaka mitatu baadae
Pamoja na mambo mengine, mkataba wa kuanzishwa kwa Jumuiya ya Afrika Mashariki unaeleza kuwa, nchi nyingine inaweza kujiunga na Jumuiya hiyo iwapo itaungwa mkono na nchi wanachama na iwapo nchi hiyo inayoomba itakuwa imetimiza masharti yafuatayo ya uongozi bora, Demokrasia, inaheshimu sheria, inasheshimu haki za binadamu, na kwamba iwe jirani na mojawapo ya nchi wanachama.
Mpaka sasa jumuiya ya Afrika Mashariki inaundwa nan chi sita, ambazo ni Kenya, Tanzania, Burundi, Rwanda, Uganda na Sudan kusini iliyojiunga mwaka 2016.