1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

DRESDEN : Schroeder arushiana vijembe na Merkel

1 Oktoba 2005
https://p.dw.com/p/CEW0

Kansela Gerhard Schroeder wa Ujerumani na mpinzani wake Angela Merkel kila mmoja amemshambulia mwenzake kuwa hafai kuiongoza Ujerumani wakati wakiwa katika kampeni ya uchaguzi wa jimbo la Dresden ambalo halikupiga kura katika uchaguzi mkuu wa Ujerumani kutokana na kufariki kwa mgombea.

Schroeder na kiongozi wa wahafidhina Merkel hapo jana waliyafikisha mapambano yao ya kutaka kuongoza katika serikali ya mseto katika mji huo wa Dresden ulioko mashariki ya Ujerumani ambapo kwa mara nyengine tena kila mmoja alidai kuwa amepata mamlaka ya kuongoza nchi kufuatia uchaguzi mkuu wa tarehe 18 mwezi uliopita wa Septemba.

Schroeder amemshutumu Merkel kwa kukosa nguvu ya kusimama kidete kwa ajili ya amani iwapo viongozi wenye ubavu duniani watajaribu kuishinikiza Ujerumani kuingia vitani.Merkel naye amesema serikali ya mseto ya chama cha Schroeder cha SPD na washirika wake wa Kijani imeondolewa madarakani kwa kura na kwamba jambo hilo linajulikana kabla ya uchaguzi huu wa Dresden na Kansela atauona ukweli huo pole pole baada ya kumalizika kwa uchaguzi huo.

Viongozi wote wawili wanawania kujisombea kura katika uchaguzi huo wa kesho mjini Dresden ili kuimarisha misimamo yao wakati wa mazungumzo ya kuunda serikali ya muungano mkuu baina ya vyama vyao ili kuweza kutekeleza mageuzi muhimu ya kiuchumi katika taifa lenye nguvu kubwa kabisa za kiuchumi Barani Ulaya.

Kila mmoja anataka kuwa Kansela katika serikali hiyo.