Droni ya Marekani yaanguka baharini, Urusi yaombwa maelezo
15 Machi 2023Taarifa kuhusu tukio hilo la kuanguka kwa droni ya kijasusi ya Marekani zilianza kuripotiwa jana jioni, kufuatia tangazo la kamandi ya jeshi la Marekani barani Ulaya.
Soma zaidi: Ukraine yadai kuishambulia meli kuu ya kijeshi ya Urusi
Katika tangazo hilo, iliarifiwa kuwa ndege mbili za kijeshi za Urusi chapa SU-27, kwa njia zinazokiuka usalama na zisizo za kiufundi, zilikatiza njia ya droni ya kiintelijensia ya Marekani chapa MQ-9 ambayo ilikuwa ikifanya operesheni zake katika eneo la kimataifa la Bahari Nyeusi.
Hatua ya mbali katika kuzidisha mivutano
Kulingana na Marekani, ndege ya Urusi ilipiga rafadha (propeller) ya droni hiyo kwa njia ambayo inakiuka kabisa sheria ya kimataifa. Mtaalamu wa masuala ya kijeshi, Thomas Wiegold ameiambia DW kwamba ingawa visa vya kukaribiana kwa vyombo vya kijeshi vya angani baina ya Urusi na Marekani vimekuwepo kwa muda, hiki cha mara hii kimekwenda mbali zaidi.
''Bila shaka marubani wa Urusi wamekuwa wakijaribu kuwabana wenzao wa Marekani na kuwalazimisha kubadilisha dira, na vimekuwepo visa vinavyohusisha vyombo vya kijasusi vya Uingereza katika anga ya Bahari nyeusi, lakini hii ni mara ya kwanza mbinu hizo zimesababisha kugongana kwa vyombo hivyo angani, na hili linaashiria hatua nyingine katika vitendo hivi vinavyozidisha mivutano,'' amesema Wiegold.
Soma Zaidi: Mashambulizi yaliyoilenga bandari ya Odessa yalaaniwa
Baadaye msemaji wa wizara ya mambo ya nje wa Marekani Ned Price alithibitisha kuwa Washington ilikuwa imemuita balozi wa Urusi Anatoly Antonov na kumtaka maelezo juu ya yaliyotokea.
Urusi yasema Marekani ndiye mchokozi
Balozi huyo hata hivyo, kupitia mtandao wa Telegram amejibu kwa kuishutumu Marekani kuichokoza Urusi. Amesema na hapa namnukuu, ''tunatarajia kwamba Marekani itajizuia kuendeleza uvumi katika vyombo vya habari na kusitisha operesheni zake katika anga ya karibu na mipaka ya Urusi, na tutachukulia vitendo vyote vinavyohusisha silaha za Marekani kama uadui wa wazi.'' mwisho wa kumnukuu.
Balozi huyo aliyekutana na naibu waziri wa mambo ya nje wa Marekani anayehusika na Ulaya Karen Donfried, alisema Urusi inataka uhusiano wa kuheshimiana kati yake na Marekani, na kwamba Urusi haitaki ugomvi baina yao.
Katika maelezo yake juu ya kilichotokea jana, wizara ya ulinzi ya Urusi imesema ilituma haraka ndege zake baada ya kugundua droni ya Marekani, na kwamba vyombo hivyo viligongana pale droni hiyo ilipobadili mwelekeo ghafla. Wizara hiyo ilisema ndege zake hazikufyatua silaha yoyote wala kukipiga chombo hicho cha Marekani.
Vyanzo: /rm, dh,zc/rc,rt, ar (AP, AFP, Reuters, dpa)