1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Dunia yaadhimisha mauaji ya halaiki ya Holocaust

27 Januari 2022

Wahanga wa mauaji ya halaiki ya Holocaust na wanasiasa wametahadharisha kuhusiana na ongezeko la chuki dhidi ya Wayahudi na watu wanaopinga kwamba kulifanyika mauaji hayo ya Holocaust.

https://p.dw.com/p/46Bxc
Berlin Bundestag Holocaust-Gedenktag  | Inge Auerbacher Überlebende
Picha: STEFANIE LOOS/AFP

Haya yanajiri wakati ambapo dunia inakumbuka uhaini uliofanywa na Wanazi siku ya Alhamis katika maadhimisho ya miaka 77 tangu kuwekwa huru kwa kambi ya mauaji ya Auschiwtz. 

Inge Auerbacher ni mhanga mwenye umri wa miaka 87 na ameliambia bunge la Ujerumani Alhamis kwamba licha ya kuwa ameishi New York, Marekani, kwa miaka 75 sasa, bado anakumbuka vyema kabisa maovu yaliyofanywa na chuki iliyokuwepo. Amesema kwa bahati mbaya chuki dhidi ya Wayahudi imeanza kuongezeka tena na ni jambo la kawaida katika nchi nyingi duniani ikiwemo Ujerumani.

Chuki dhidi ya Wayahudi iko katika jamii

Spika wa bunge la Ujerumani Baerbel Bas ameliambia bunge Alhamis kwamba janga la virusi vya corona limekuwa kama kichocheo cha chuki dhidi ya Wayahudi ambayo tayari ni tatizo kubwa Ujerumani.

Berlin Bundestag Holocaust-Gedenktag  | Baerbel Bas
Spika wa bunge la Ujerumani, Bundestag, Baerbal BasPicha: Stefanie Loos/AFP

"Chuki dhidi ya Wayahudi iko - haiko tu miongoni mwa watu wachache au matusi machache mitandaoni. Ni tatizo la jamii yetu - jamii nzima. Chuki dhidi ya Wayahudi iko miongoni mwetu," alisema Bas.

Spika wa bunge la Israel Mickey Levy amebubujikwa na machozialipokuwa akikariri sala ya Kiyahudi ya maombolezo kutoka kwenye kitabu cha mvulana mmoja wa Kiyahudi aliyekuwa akiishi Ujerumani.

Levy amesema Israel na Ujerumani zimepitia safari ngumu ya utangamano na zimekuwa na urafiki wa kijasiri.

"Ujerumani na Israel zimejenga daraja. Zinaona umuhimu wa demokrasia sawa sawa na wanajua umuhimu wa kushirikiana kuhifadhi demokrasia hiyo," alisema Levy.

Jumla ya watu milioni 6 waliuwawa

Kutokana na janga la virusi vya corona, hafla nyingi za makumbusho ya mauaji hayo ya halaiki zinafanyika mitandaoni mwaka huu kwa mara nyengine.

Lakini katika eneo kulikokuwa na kambi ya mauaji ya Auschwitz kunafanyika sherehe ndogo ya makumbusho. Vikosi vya wanajeshi wa Kinazi wa Ujerumani waliokuwa wanapigana katika Vita vya Pili vya Dunia, waliwauwa watu milioni 1.1 katika kambi hiyo nchini Poland.

Kwa ujumla, karibu Wayahudi milioni 6 waliokuwa wanaishi Ulaya na mamilioni ya watu wengine waliuwawa na Wanazi na washirika wao katika kipindi cha Holocaust. Kati ya hao waliouwawa, milioni 1.5 walikuwa watoto.

Vyanzo/APE/AP