Duru ya nane ya mazungumzo ya nyuklia na Iran yaanza Vienna
28 Desemba 2021Mwanadiplomasia wa Umoja wa Ulaya anayeongoza mazungumzo hayo Enrique Mora amesema pande zote zinazohudhuria majadiliano ya mjini Vienna zimeonesha wazi nia ya kutaka kupata mafanikio lakini mashauriano katika siku zijazo yatakuwa magumu.
Mora amewaambia waandishi habari kwamba wanajitayarisha kufanya kazi kwa umakini mkubwa katika duru hiyo ya nane ya mazungumzo baada ya awamu nyingine saba zilizotangulia kushindwa kumaliza utata na mivutano katika masuala kadha.
Duru ya saba ya mazungumzo, iliyokuwa ya kwanza chini ya serikali mpya ya wahafidhina nchini Iran, ilimalizika siku 10 zilizopita kwa kuongeza matakwa kadhaa ya Iran katika hati ya mashauriano.
Kwa muda sasa mataifa ya magharibi yanasema mazungumzo ya mjini Vienna yanajikokota na kwa sehemu fulani yanavunja moyo huku wanadiplomasia wake wakionya kuwa muda ni mchache wa kufikia makubaliano kabla mkataba huo wa nyuklia wa mwaka 2015 kupoteza umuhimu wake.
Iran haipepesi macho juu ya kile inachotaka
Ujumbe wa Iran uko mjini Vienna kwa lengo mahsusi safari hii na umelisema waziwazi.
Taifa hilo la Uajemi linataka ajenda kuu ya majadiliano ya duru ya nane iwe ni kutafuta uhakika wa Iran kuondolewa vikwazo vya kiuchumi bila ya masharti na Marekani iseme kinagaubaga kuwa inarejea ndani mkataba huo wa nyuklia iliyojitoa mwaka 2018.
Akizungumza kabla ya kuanza kwa mazungumzo mjini Vienna msemaji wa wizira ya mambo ya kigeni wa Iran Saeed Khatibzadeh alisema "Tunawashauri washiriki wote kuja mjini Vienna wakiwa na azma ya kupata makubaliano mazuri. Kisichokubalika upande wa Iran ni ukweli kwamba baadhi ya washiriki wanadhani wanaweza kupoteza muda na nguvu za wengine kwa kutumia kampeni za kupalilia uongo au kuvuruga ukweli"
Moja ya kizingiti kinachoandama mazungumzo yanayoendelea ni msimamo wa Iran wa kupinga kukutana ana kwa ana na maafisa wa Marekani na kwa hivyo kulazimisha washiriki wengine kuwa wajumbe wa kusafirisha taarifa kati ya pande hizo mbili.
Marekani inayohimizwa kurejea kwenye mkataba huo wa nyuklia imesema utaratibu huo ni wa polepole na unatatiza kusonga mbele kwa mazungumzo.
Washington: Shuguli za nyuklia za Iran zinaleta wasiwasi
Washington pia na washirika wake wa magharibi wanaituhumu Tehran kwamba inafanya mchezo wa kupoteza muda ikitiliwa maanan kwamba shughuli zake za Iran zinazoendelea zinatia wasiwasi.
Hivi karibuni shirika la kudhibiti nguvu za Atomiki la Umoja wa Mataifa IAEA lilisema linatiwa mashaka na kuongezeka kwa hifadhi ya madini ya Urani yaliyorutubishwa nchini Iran.
Hata hivyo siku ya Jumamosi mkuu wa shirika la nguvu za atomiki la Iran Mohammad Eslami alisema nchi hiyo haina mipanyo ya kuongeza urutubishaji madini ya Urani kwa zaidi ya asili 60 hata ikiwa mazungumzo ya mjini Vienna hayatazaa matunda.