EAC yatangaza mazungumzo ya amani kwa Congo Mashariki
14 Novemba 2022Tangazo hilo la jumuiya ya Afrika Mashariki, EAC, lilikuja wakati vikosi vya jeshi la Congo vikipambana upya na waasi wa M23 kaskazini mwa mji mkuu wa mkoa tete wa Kivu Kaskazini, walisema maafisa.
Duru za kijeshi zilisema jeshi lilikabiliana na M23 katika kijiji cha Mwaro, kilichoko umbali wa kilomita 20 kaskazini mwa mji huo ambao ni kitovu cha kibiashara na nyumbani kwa watu milioni moja.
"Tuliamkia mapigano asubuhi hii," alisema afisa mmoja wa jeshi katika mazungumzo na shirika la habari la AFP.
Soma pia: Vijana wengi wa mkoa wa Kivu Kaskazini kujiandikisha jeshini
Mwingine alisema hali ilikuwa ngumu, kukiwa na wapiganaji wa M23 waliouawa "kwa wingi" lakini pia kuna vifo kwa upande wa jeshi la Congo.
Makabiliano makali yalidumu hadi Jumapili usiku huko Kibumba, ambalo ni eneo jengine la makaazi lililoko umbali wa kilomita 20 kutoka Goma, kwa mujibu wa wakaazi na maafisa wa usalama.
Waasi wa M23 wameibuka hivi karibuni kote katika mkoa wa DRC wa Kivu Kaskazini, wakipata ushindi kadhaa dhidi ya jeshi na kuteka maeneo makubwa ya ardhi.
Siku ya Jumamosi, kundi lililituhumu jeshi la Congo kujibu mashambulizi kwa kutumia "mabomu ya kifedhuli"-- na kuua raia 15, wakiwemo watoto wawili. Shirika la AFP halikuweza kuthibitisha idadi hiyo ya vifo.
Vurugu hizo za karibuni zaidi zinakuja siku moja baada ya wanajeshi wa Kenya kupelekwa mashariki mwa DRC, kama sehemu ya operesheni ya kulinda amani kutoka jumuiya ya Afrika Mashariki.
Soma pia: DRC, Rwanda zakubaliana kusaka suluhisho
Kundi la M23 ambalo lina wapiganaji wengi wa kabila wa Watutsi, lilijitokeza kwa mara ya kwanza mwaka 2012 lilipouteka kwa muda mfupi mji wa Goma kabla ya kufurushwa na kujichimbia.
Kundi hilo liliibuka tena mwishoni mwa 2021, na kuanzisha tena mapambano kwa madai kwamba DRC ilishindwa kutimiza ahadi yake ya kuwajumuishwa jeshini, miongoni mwa malalamiko mengine.
Kuibuka tena kwa M23 kumesababisha kuvurugika kwa uhsuiano kati ya DRC na jirani yake mdogo zaidi Rwanda, ambayo Kinshasa inaishtumu kwa kuunga mkono wapiganaji hao.
Licha ya ukanushaji rasmi kutoka Kigali, ripoti ambayo haijachapishwa ya Umoja wa Mataifa ambayo shirika la AFP lilipata nakala yake mwezi Agosti, imetaja ushiriki wa Rwanda katika M23.
Juhudi za kikanda kutatua mzozo
Kinshasa ilimtimua balozi wa Rwanda mwishoni mwa mwezi Oktoba, wakati M23 ikiteka maeneo zaidi, huku ikimuita balozi wake kutoka Kigali. Msuguano huo umepelekea juhudi kadhaa za kidiplomasia kutatua mzozo.
Rais wa Angola Joao Lourenco alikurana na rais wa Congo Felix Tshisekedi katika mji mkuu wa Congo siku ya Jumamosi, kwa mfano, baada ya kuzuru Rwanda siku iliyotangulia.
Siku ya Jumapili, rais wa zamani wa Kenya Uhuru Kenyatta, mpatanishi wa EAC katika mzozo huo, aliwasili pia Kinshasa kwa mazugumzo.
Soma pia: DRC yaahidi kukomboa maeneo yanayodhibitiwa na waasi wa M23
EAC ilisema Jumapili itafanya mazungumzo yenye lengo la kuleta amani mashariki mwa Congo mjini Nairobi mwezi huu. Haikubainisha nani atashiriki mazungumzo hayo wala muda gani yamepnagiwa kudumu.
Juhudi hizo za amani zinakwenda sambamba na juhudi za kijeshi kurejesha utulivu mashariki mwa DRC.
Mnamo mwezi Aprili, viongozi wakuu wa EAC walikubaliana kuunda kikosi cha pamoja kusaidia kurejesha usalama katika taifa hilo lenye utajiri wa madini.
Wanajeshi wa Kenya walianza kuwasili mjinim Goma mwishoni mwa wiki kama sehemu ya kikosi hicho, baada ya bunge la nchi hiyo kuidhinishwa kupelekwa kwa wanajeshi zaidi ya 900, kwa kipindi cha awali cha miezi sita.
Wakati kikosi hicho kitakuwa chini ya kamandi ya Kenya, ukubwa wake jumla ya upana vinasalia kutokuwa wazi.
Chanzo: AFPE