1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

ECOWAS kukutana na viongozi wa Mali wanaoshikiliwa

26 Mei 2021

Wapatanishi wa Afrika Magharibi Jumatano wanatarajiwa kukutana na viongozi wa serikali ya mpito ya Mali ambao wanashikiliwa, siku mbili baada ya viongozi hao kuondolewa madarakani na jeshi.

https://p.dw.com/p/3tyO4
Mali politische Krise | Vermittler Goodluck Jonathan aus Nigeria
Picha: Getty Images/J. Kalapo

Duru karibu na mazungumzo hayo zimeeleza kuwa Rais Bah Ndaw na Waziri Mkuu Moctar Ouane watakutana na ujumbe wa upatanishi wa Jumuiya ya Uchumi ya nchi za Afrika Magharibi, ECOWAS, uliowasili jana kwenye mji mkuu wa Mali, Bamako.

Kiongozi wa jeshi, Kanali Assimi Goita aliyewaondoa madarakani viongozi hao waliopewa jukumu la kuiongoza serikali ya mpito iliyowekwa mwezi Agosti mwaka uliopita na kuhakikisha kurejea kwa utawala wa kiraia baada ya mapinduzi, amesema ujumbe wa ECOWAS umeruhusiwa kukutana na kufanya mazungumzo na Ndaw na Ouane.

ECOWAS kusaidia kupatikana suluhisho

Kiongozi wa ujumbe huo, rais wa zamani wa Nigeria, Goodluck Jonathan amesema wameenda Bamako kuwasaidia ndugu zao wa Mali kupata suluhisho la mzozo huo, lakini ni wazi ECOWAS inaweza kuiwekea vikwazo katika mkutano ujao wa kilele.

"Kwa kweli tuko hapa sababu kuna masuala kadhaa ambayo ECOWAS ina wasiwasi nayo kidogo, na kama timu inayopatanisha tunahitaji kuja kuwasikiliza watu wetu. Hatuwezi kusema chochote hadi tutakapofanya mazungumzo na vyama vya kiraia, wananchi wa Mali, jeshi na wale waliokuwepo kwenye serikali. Baada ya mazungumzo haya basi tutakuwa na kitu cha uhakika cha kuvieleza vyombo vya Habari," alifafanua Jonathan.

Mali | Interimspräsident Bah Ndaw
Rais Bah Ndaw anayeshikiliwa na jeshiPicha: Amadou Keita/Reuters

Siku ya Jumatatu katika hali isiyo ya kawaida Umoja wa Mataifa, Umoja wa Afrika, ECOWAS, Umoja wa Ulaya na Marekani zilitoa taarifa ya pamoja kulaani kitendo hicho na kutoa wito kwa viongozi hao kuachiwa mara moja bila masharti yoyote yale.

Afisa wa ngazi ya juu wa Mali ambaye hakutaka kutajwa jina lake, amesema Ndaw na Ouane wamepelekwa katika kambi ya kijeshi ya Kati karibu na Bamako na kwamba wanaendelea vizuri. Amesema viongozi hao walilala sehemu nzuri na rais aliruhusiwa kuonana na daktari wake.

Soma zaidi: Viongozi wa Mali washikiliwa na jeshi

Wakati huo huo, Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa Jumatano litafanya mkutano wa dharura na wa faragha kuhusu Mali. Mkutano huo umependekezwa na Ufaransa, Niger, Tunisia, Kenya pamoja na Saint Vincent na Grenadines.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Ufaransa, Jean-Yves Le Drian alitangaza awali mjini Paris kwamba ombi la kufanyika kikao maalum cha Baraza hilo lilipelekwa baada ya mapinduzi kutokea Mali, bila ya kufafanua lini kitafanyika. Hata hivyo, hakuna dalili kuhusu uwezekano wa kupitishwa kwa tamko la pamoja katika mkutano huo wa dharura.

Katika hatua nyingine, China imezitaka pande zinazohasimiana Mali kumaliza tofauti zao kupitia njia ya mazungumzo ili kudumisha utulivu na umoja wa kitaifa.

(AFP, Reuters)