1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

El-Chapo afungwa maisha

17 Julai 2019

Mlanguzi wa kimataifa wa dawa za kulevya Joaquin "El Chapo" Guzman amehukumiwa kifungo cha maisha jela pamoja baada ya kukutikana na hatia ya kuendesha genge la mauaji ya kihalifu.

https://p.dw.com/p/3MD1u
Mexiko, Mexiko City: Joaquin "El Chapo" Guzman
Picha: picture-alliance/AP/E. Verdugo

Hukumu hii inachukuliwa kama hitimisho la hujuma hiyo ya muda mrefu iliyofanywa na genge hilo la El Chapo.

Kulingana na mwendesha mashitaka, hukumu ya kesi hiyo inayosikilizwa na mahakama ya serikali kuu ya Brooklyn inatarajiwa kuangazia kisa cha mtu mmoja aliyearifu kwamba alinusurika kuuawa katika shambulizi lililopangwa na Guzman. Jina la mtu huyo halikutajwa hadharani.

Mnamo mwezi Februari, Guzman, 62 alikutwa na hatia ya kufanya biashara haramu ya maelfu ya tani ya dawa za kulevya aina ya cocaine, heroin na bangi, pamoja na kujihusisha na kupanga matukio kadhaa ya mauaji, wakati akiwa kama kiongozi wa genge la Sinaloa, ambalo kwa muda mrefu lilitambulika kuwa genge kubwa zaidi miongoni mwa mengine, lenye ubabe na linalouza madawa kwa wingi zaidi.

Waendesha mashitaka wamemuomba jaji wa mahakama ya wilaya Brian Cogan kumuhukumu kifungo cha maisha gerezani, pamoja na miaka 30 ya kutumia silaha za moto. Mawakili wa Guzman bado hawajajadiliana kuhusu ulazima wa adhabu hiyo kulingana na mashitaka ya mteja wao.

USA Mexikanischer Drogenboss «El Chapo» muss lebenslang ins Gefängnis
Mkewe El Chapo(mwenye miwani ya jua katikati) akitoka mahakani baada ya hukumu ya mumewe. Picha: Reuters/B. McDermid

Guzman ambaye jina lake linamaanisha "Mfupi" aliwahi kujizolea umaarufu mkubwa kwenye eneo la jimbo lake la Sinaloa, alikozaliwa. Alizaliwa kwenye makazi masikini yaliyoko katika kijiji kilichoko milimani.

Aliwahi kutoroka mara mbili gerezani.

Amekuwa kizuizini, katika chumba alichofungiwa peke yake kwenye gereza la Metropolitan, lenye muundo wa ngome huko Manhattan. Mwezi uliopita, jaji Cogan alitupilia mbali ombi la Guzman la kufanya mazoezi kwenye dari ya gereza hilo, baada ya waendesha mashitaka kusema anaweza kutumia upenyo huo kutoroka.

Kabla ya kukamatwa mwaka 2016, Guzman alifanikiwa kutoroka mara mbili kwenye magereza yenye ulinzi mkali nchini Mexico. Alirejeshwa Marekani kukabiliana na mashitaka dhidi yake mwezi Januari, 2017.

Guzman, alijitangazia umaarufu wa jina lake kama mfanyabiashara wa dawa hizo za kulevya miaka ya 1980, wakati alipochimba mahandaki katika mpaka wa Mexico, ya kupitisha na kufanya biashara hiyo kwa haraka zaidi kuliko wapinzani wake wa kibiashara.

Alijiimarisha zaidi kibiashara katika miaka ya 1990 hadi 2000, kupitia vita vya mara kwa mara na wapinzani wake, na hatimaye kuja kujulikana zaidi kama kiongozi wa genge hilo la Sinaola.

Kesi yake iliyosikilizwa kwa wiki 11, ilikwenda sambamba na ushahidi kutoka kwa washirika wake kadhaa, waliokubaliana na waendesha mashitaka kutoa ushirikiano, walioelezea kwa kina namna genge hilo lilivyokuwa likifanya shughuli zake. 

Jaji huyo wa Marekani amedai kwamba Guzman aliuza madawa ya thamani ya zaidi ya dola bilioni 12, na gazeti la Forbes liliwahi kumuorodhesha kama mmoja ya watu matajiri zaidi duniani.