1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

EU yatafakari vikwazo vipya kufuatia kifo cha Navalny

20 Februari 2024

Umoja wa Ulaya umeapa kuiwajibisha Moscow baada ya kifo cha kiongozi wa upinzani Alexei Navalny. Brussels pia inatafakari vikwazo vipya kuhusiana na vita vyake nchini Ukraine.

https://p.dw.com/p/4cb1I
Reaktionen auf den Tod von Alexej Nawalny
EU inasema kifo cha Navalny ni dalili nyingine ya ukandamizaji wa kimfumo nchini Urusi Picha: Beata Zawrzel/ZUMAPRESS/picture alliance

"aliuawa taratibu katika gereza la urusi na utawala wa Putin.”

Hayo ndio maneno aliyotumia mkuu wa sera za kigeni wa Umoja wa Ulaya kumuelezea Alexei Navalny, mwanasiasa wa upinzani wa Urusi aliyeripotiwa kufariki wiki iliyopita. Mawaziri wa Umoja wa Ulaya walifanya mazungumzo na mjane wa Navalny, Yulia Navalnaya mjini Brussels Jumatatu, wakiahidi uungaji mkono wao baada ya kumtuhumu Rais wa Urusi Vladmir Putin kwa kusababisha kifo cha mumewe gerezani.

Gereza alilokuwa anazuiliwa Navalny
Navalny aliripotiwa kufariki katika gereza la KharpPicha: AP/dpa/picture alliance/

"Kifo kisichotarajiwa na cha kushtusha cha Bw Navalny ni ishara nyingine ya ukandamizaji wa kimfumo unaoongeza kasi nchini Urusi." Umoja huo umesema katika taarifa. "EU itatumia juhudi zozote za kuwawajibisha viongozi wa kisiasa wa Urusi na mamlaka, kwa uratibu wa karibu na washirika wetu; na kuwawekea gharama zaidi kwa hatua zao, pamoja na kupitia vikwazo."

Borrell hakutoa ratiba wala maelezo ya vikwazo hivyo, ambavyo kuna uwezekano vitahusisha ukamataji wa mali na marufuku ya kusafiri dhidi ya watu au mashirika yanayotuhumiwa kuhusika katika kifo cha Navalny.

Hayo yalijiri wakati wa mkutano wa mawaziri wa mambo ya nje wa nchi 27 wanachama, ambao ulikuwa umepangwa kabla ya kifo cha Navalny, ili kujadili vikwazo vipya ikiwa ni miaka miwili tangu Urusi ilipofanya uvamizi kamili nchini Ukraine mnamo Februari 24.

Waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani Annalena Baerbock amesema anatumai Umoja wa Mataifa utakubaliana hivi karibuni kuhusu kifurushi cha vikwazo vipya.

Waziri wa mambo ya kigeni wa Hungary Peter Szijjarto alisema kutangaza vikazo zaidi vya Umoja wa Ulaya dhidi ya Urusi hakuingii akilini na kuwa kutauharibu tu Uchumi wa jumuiya hiyo. Lakini aliongeza kuwa Budapest haitapinga vikwazo hivyo.

Mjane wa Navalny, Yulia Navalnaya katika makao makuu ya EU Brussels
Yulia amesema Rais Putin ndiye alimuuwa mumewePicha: Yves Herman/AP/picture alliance

Mabalozi wa Urusi waitwa

Mabalozi wa Urusi wameitwa kote barani Ulaya kujibu maswali kuhusu kifo cha kiongozi maarufu wa upinzani nchini Urusi Alexei Navalny. Ujerumani, Sweden, Finland na mataifa ya Baltiki ni miongoni mwa mataifa yaliyowaita mabalozi wa Urusi kwa mazungumzo ya dharura wakati kukiwa na hofu kuwa kifo cha Navalny kinahusishwa na uchaguzi wa rais unaopangwa Machi nchini Urusi, ambao Putin anatarajiwa kushinda kwa mara nyingine kwa kishindo.

Yulia Navalnaya, aliapa kuendeleza kazi aliyoancha mumewe ya kupambania uhuru wa nchi yake huku akitoa wito kwa wafuasi wake kuendelea kumuunga mkono. Alisema Rais Putin ndiye aliyemuua mumewe.

Maafisa wa Urusi, ambao bado hawajauachia mwili wa Navalny au kutoa ripoti ya uchunguzi tangu kifo chake Ijumaa iliyopita, wamewakamata watu waliokuwa wakishiriki hafla za kutoa heshima zao kwa mkosoaji huyo mkubwa wa Kremlin.

Reuters, afp