EU yawaita viongozi wa Serbia na Kosovo kwa mazungumzo
22 Juni 2023Umoja wa Ulaya umewaita viongozi wa Serbia na Kosovo kwa mazungumzo ya dharura ya kujaribu kumaliza msururu wa mashambulizi yanayochochea hofu ya kurejea kwa mzozo baina yao.
Soma pia: Kosovo yaruhusu magari ya Serbia na bidhaa kuvuka mpaka tena
Mkuu wa Sera za Kigeni wa Umoja wa huo, Josep Borrell, amesema atafanya mkutano wa dharura na Waziri Mkuu wa Kosovo Albin Kurti na Rais wa Serbia, Aleksandar Vucic, mjini Brussels, ingawa haikufahamika iwapo wakuu hao wawili watakutanishwa ana kwa ana ama atazungumza nao kwa nyakati fofauti.
Wasiwasi uliibuka upya mwezi uliopita baada ya polisi wa Kosovo kulikamata jengo la manispaa ya kaskazini mwa nchi hiyo inayokaliwa na idadi kubwa ya Waserbia, ambao waliwaweka mameya wenye asili ya Albania, waliochaguliwa kwenye uchaguzi ambao, hata hivyo, ulisusiwa na idadi kubwa ya Waserbia.