Euro 2020: Italia yaitandika Uturuki bao 3-0
12 Juni 2021Timu ya taifa ya soka ya Italia maarufu kama Azzurri imefungua pazia ya michuano ya kandanda barani Ulaya euro 2020 kwa ushindi mnono wa mabao 3-0 dhidi ya Uturuki katika dimba la Stadio Olimpiko mjini Roma.
Ikicheza mara ya kwanza katika michuano mikubwa ndani ya kipindi cha miaka mitano baada ya kushindwa kufuzu katika kombe la dunia la mwaka 2018, Italia ilifanikiwa kupachika magoli yote matatu katika kipindi cha pili mchezo katika dimba la Stadio Olimpico ambalo lilijazwa na mashabiki karibu robo ya uwezo wake.
Bao la kujifunga la mchezaji wa Uturuki Merih Demiral liliiweka Italia mbele kabla ya Ciro Immobile na Lorenzo Insigne kupachika mabao mengine mawili na kuiweka vizuri Italia katika ufunguzi wa kundi A.
Ushindi huo umehitimisha usiku uliojawa na hisia kubwa na shamrashamara katika mji mkuu wa Italia Roma, ambao umeshuhudia mashabiki 16,000 wakiruhusiwa kuingia uwanjani.
Kocha wa Italia Roberto Mancini ambaye amekiimarisha kikosi hicho baada ya kushindwa kufuzu michuano ya kombe la dunia ya 2018 nchini Urusi amesema "wamecheza vizuri".
"Kwa kuzingatia ilikuwa mechi ya kwanza, haikuwa rahisi na tulicheza dhidi ya timu nzuri. Umati wa mashabiki umetusaidia, na ilikuwa muhimu kwetu kucheza kandanda safi", amesema Mancini mara baada ya mechi.
Kiungo wa kati wa Uturuki Kenan Karaman alisema kuwa wameipatia Italia nafasi nyingi katika kipindi cha pili na hivyo kupoteza mchezo.
Hafla ya ufunguzi wa michuano hiyo ambayo ilikuwa imeahirishwa kwa mwaka mmoja kutokana na janga la virusi vya corona, ilitawaliwa na shangwe zilizoambatana na fataki na mataa yaliyoupamba vyema uwanja wa olimpico.
Wachezaji wa zamani wa kikosi cha Italia kilichoshinda kombe la dunia Alessandro Nesta na Francesco Totti, ambao walikipiga katika klabu za Lazio na Roma, walibeba mpira katikati ya dimba la Stadio Olimpico kabla ya kuanza kwa mechi.
Italia ilionyesha kutawala mchezo kipindi cha mwanzo kwa kufanya mashambulizi kadhaa yaliyoongozwa na Immobile anayechezea klabu ya Lazio. Italia imeshinda kombe la Ulaya mara moja mwaka 1968 huku Uturuki ikifanikiwa kufika hatua ya nusu fainali ya michuano ya ulaya mwaka 2008.
Wales na Uswisi zinakutana baadae leo mjini Baku Azerbaijan. Siku ya Jumatano, Italia itakutana na Uswisi mjini Roma, Uturuki itavaana na Wales huko Baku katika raundi ya pili ya mechi za kundi A.
Leo pia zitachezwa mechi za kundi B ambapo Denmark anavaana na Finland mjini Copenhagen na Ubelgiji inavaana uso kwa uso na Urusi huko St Petersburg. Michuano ya kombe la EURO 2020 inafanyika katika nchi 11 na mashabiki watapaswa kufunga safari katika nchi mbalimbali kwa ajili ya kushuhudia mechi.