1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Euro 2020: Nani mkali kati ya Ujerumani na Ufaransa?

15 Juni 2021

Timu za taifa za Ujerumani na Ufaransa kawaida hukutana katika hatua za mwisho mwisho za mashindano makubwa ya soka, lakini sio mara hii.

https://p.dw.com/p/3uxc4
UEFA EURO 2016 - Halbfinale | Frankreich vs. Deutschland - Emre Can & Blaise Matuidi
Picha: Getty Images/A. Livesey

Timu za taifa za Ujerumani na Ufaransa kawaida hukutana katika hatua za mwisho mwisho za mashindano makubwa ya soka, lakini sio mara hii.

Timu hizo zitakutana katika hatua ya makundi ya mashindano ya mataifa ya Ulaya kwa mara ya kwanza leo Jumanne (Juni 15) wakati wa mechi ya ufunguzi ya Kundi F la michuano ya Euro 2020 mjini Munich.

Mechi ya mwisho kwa timu hizo mbili kukutana ilikuwa kwenye mashindano ya Euro 2016 katika hatua ya nusu fainali, ambapo Antoine Griezmann aliifungia Ufaransa mabao mawili katika ushindi wa 2-0.

Tangu wakati huo, timu ya taifa ya Ujerumani imeandikisha matokeo yasiyoridisha kuelekea mchezo wa leo kinyume na Ufaransa ambayo miaka miwili baadaye ilishinda Kombe la Dunia.

Cha kushangaza ni kuwa hakuna mchezaji yeyote katika kikosi cha sasa cha Ujerumani ambaye amewahi kufunga bao katika mashindano ya Ulaya. Thomas Mueller, ambaye amecheza mechi 11 za mashindano ya Ulaya, alikosa penalti katika hatua ya robo fainali walipoifunga Italia kupitia mikwaju ya penalti.

Ujerumani inatarajia kuanza vizuri mchezo wa leo mjini Munich na kuiga mafanikio waliyoyapata katika Kombe la Dunia la mwaka 2014. Mashindano haya yatakuwa ya mwisho kwa Joachim Loew kama kocha baada ya kuitia makali timu ya taifa ya Ujerumani, Die Mannschaft, kwa muda wa miaka 15.

UEFA EURO 2016 - Halbfinale | Frankreich vs. Deutschland
Wachezaji wa timu ya taifa ya Ufaransa wakisheherekea baada ya kuibandua nje Ujerumani kwenye michuano ya Euro 2016Picha: Reuters/K. Pfaffenbach

Aliyekuwa naibu wake, Hansi Flick, atachukua mikoba ya kuinoa timu hiyo baada ya mashindano ya Euro na atakuwa na jukumu la kuiongoza timu hiyo kutafuta tiketi ya kufuzu kwa Kombe la Dunia mwakani nchini Qatar.

Loew alisema siku ya Jumatatu (Juni 14) kuwa maandalizi ya timu yamekamilika vizuri kuelekea mchezo wa leo.

"Wachezaji wamejiandaa vizuri, vizuri tena sana. Kila mtu ana hamu ya kupata mafanikio katika michuano hii ya Euro na kwa kweli hilo limenifanya mimi kujiamini na kuniruhusu nilale vizuri," alisema Loew.

Loew, ama Jogi kama anavyojulikana kwa jina la utani, alisema kiungo wa Bayern Munich, Leon Goretzka, atakuwa yuko tayari kucheza japo hatokuwa fiti katika mchezo wa leo dhidi ya Ufaransa. Jonas Hofmann, ndiye mchezaji pekee majeruhi.

Ujerumani pia itachuana na mabingwa watetezi Ureno mnamo Juni 19, siku nne tu kabla ya kucheza mechi yao ya mwisho na Hungary. Die Mannschaft itacheza mechi zake zote tatu za makundi mjini Munich.

Katika mechi nyengine za leo za Kundi F, Hungary itakuwa na miadi na mabingwa watetezi Ureno katika uwanja wa Puskas mjini Budapest.

Loew aliwajumuisha wachezaji wazoefu, Thomas Mueller na Mats Hummels, kwenye mashindano ya mwaka huu na uzoefu wao umeonekana kukiimarisha kikosi hicho.

Hata hivyo, Ujerumani itatakiwa kuwa makini kuikabili safu ya ushambuliaji ya Ufaransa wakiwemo Antoinne Griezmann, Kylian Mbappe na Karim Benzema, aliyeitwa kikosini baada ya kutokuwepo kwa miaka sita. Watatu hao huenda wakatumia mianya ya kuregarega kwa safu ya ulinzi ya Ujerumani.

Ujerumani inawania kuwa nchi ya kwanza kushinda Kombe la Dunia na Michuano ya Mataifa ya Ulaya ya Euro kwa wakati mmoja.

Kocha wa Ufaransa, Didier Deschamps, alishinda Kombe la Dunia akiwa mchezaji mnamo mwaka 1998 na kombe la Euro la mwaka 2000 na huenda akashinda tena mataji hayo japo wakati huu kama kocha.

Kando na Ufaransa, timu za taifa za Ujerumani Magharibi na Uhispania pia zimewahi kushinda Kombe la Dunia na Kombe la Euro kwa wakati mmoja.