Fainali EURO 2020: Vita vitakuwa kati ya manahodha
10 Julai 2021Jumapili ndiyo itakayokuwa mara ya kwanza "the Three Lions" kama wanavyofahamika England kwa utani, watakapocheza mechi ya fainali tangu waliposhinda Kombe la Dunia mwaka 1966, hilo likiwa ni pengo la miaka 55 kabla kucheza fainali.
Kwa mara ya kwanza England watakuwa wanacheza kwenye fainali ya mashindano ya Kombe la Ulaya huku Italia wakiwa walishinda kombe hilo mwaka 1968 na mwaka 2000 na 2012 wakaishia kumaliza katika nafasi ya pili. Katika mechi sita walizocheza na Italia, England hawajashinda hata moja, wametoka sare mbili na kufungwa nne.
Mara ya mwisho kuwafunga Italia ilikuwa mwaka 1978 katika mechi za kuwania kutinga Kombe la Dunia waliopata ushindi wa 2-0. Lakini hayo yalipita, wacha tugange haya ya kesho, je, kinyang'anyiro kikuu kitakuwa wapi kwenye mechi ya kesho?
Kane na Chiellini walipambana mara ya kwanza 2015
Mshambuliaji na nahodha wa England Harry Kane anakutana tena na hasimu wake wa zamani beki mzoefu na nahodha wa Italia Giorgio Chiellini. Kane amepitia mengi kama mchezaji chipukizi tangu alipopambana na Chiellini kwa mara ya kwanza mwaka 2015 ila Muitaliano huyo, licha ya jua la umri katika usakataji kandanda kuelekea kutua, bado yuko imara sana.
Italia ilipambana na England mjini Turin Italia Machi 2015 na kwa mara ya kwanza kabisa Harry Kane akapewa nafasi ya kuichezea timu yake ya taifa katika kikosi cha kwanza, kwa mara ya kwanza kabisa baada ya kung'ara katika mechi ya awali walipocheza na Lithuania. Katika mechi hiyo na Italia Kane aliyekuwa na umri wa miaka 21, alipambana na mmoja wa mabeki bora zaidi duniani Giorgio Chiellini na alikuwa na wakati mgumu si haba. England waliishia kupata sare ya bao moja katika mchuano huo.
Mwaka 2018, klabu ya Kane, Tottenmham Hotspur ilipatana na Juventus katika mechi ya vilabu bingwa barani Ulaya ungwe ya 16 bora na Juve wakawabandua Spurs kwa jumla ya magoli 4-3 ila Kane alionyesha kwamba amekomaa mbele ya Chiellini kwani alitikisa wavu huko Turin.
Romelu Lukaku alidhibitiwa na mabeki wa Italia, Harry Kane atafurukuta?
Sio kusema kwamba Chiellini ni mchezaji aliyekamilika sana, la hasha, kulikuwa na minong'ono Italia kikosi cha timu ya taifa kilipotajwa na Chiellini kujumuishwa wengi wakidai kwamba nyota huyo mwenye miaka 36 hatoweza kupambana na vijana wenye damu za kuchemka tena, ila minong'ono hiyo sasa imetulia kutokana na mchezo wa kuridhisha aliouonyesha hadi kufikia sasa.
Kane ni mchezaji ambaye kwa sasa yuko katika kilele cha mchezo wake na anafurahia kila dakika uwanjani ila jinsi mabeki wa Italia walivyomnyamazisha mchezaji mwengine ambaye kwa sasa ni moto mbele ya wavu, namzungumzia Romelu Lukaku, Ubelgiji walipobanduliwa na Italia kwenye robo fainali, ni jambo ambalo linastahili kumfanya Kane ajifikirie mara mbili.
Bila shaka mpambano kati ya manahodha hawa wawili ni mpambano utakaoamua ni nani atakayenyanyua ubingwa wa mataifa ya Ulaya baada ya dakika 90, 120 au hata baada ya mikwaju ya penalti.