Familia nyingi hazimudu gharama za kutibu Saratani
4 Februari 2021Kwa sasa ni vituo vitatu pekee vya umma vya afya vinavyotoa tiba ya mionzi kwa wagonjwa. Kiasi ya watu alfu 35 wanafariki kila mwaka nchini humo kwa sababu ya saratani.
Maadhimisho ya saratani nchini Kenya yamefanyika kwa njia ya mtandao ambapo kikao hicho kiliwaleta pamoja wadau wa kupambana na saratani na waziri wa afya Mutahi Kagwe. Kwa upande mwengine, kwenye uzinduzi wa ripoti hiyo iliyoandaliwa na Benki ya Dunia na Wizara ya afya nchini Kenya, mkuu wa kitengo cha kitaifa cha kupambana na saratani Dr Mary Nyangasi aliusisitizia umuhimu wa kupimwa mapema ili kuiondoa haja ya tiba za ghali pale ugonjwa utakapokuwa umesambaa.Hata hivyo kikwazo ni uhaba wa vituo vya umma vya afya vya vipimo.Kauli hizo zinaungwa mkono na David Makumi ambaye ni mwenyekiti wa mashirika yanayopambana na saratani nchini Kenya,KENCO.
Takwimu zinaonyesha kuwa asilimia 22 ya hospitali za umma ndizo zilizo na uwezo wa kutoa huduma za vipimo vya saratani kote nchini. Hali ni mbaya kwenye hospitali kuu ya rufaa ya Kenyatta ya hapa jijini Nairobi, ambapo wagonjwa wa saratani hulazimika kusubiri kwa mwezi mmoja au zaidi kabla ya kupata huduma za tiba ya mionzi.
Msongamano mkubwa kadhalika unaripotiwa kutokea kwenye hospitali ya rufaa ya chuo kikuu cha Kenyatta kwani wagonjwa ni wengi.Wakati huohuo ripoti hiyo ya benki ya dunia na wizara ya afya imebaini kuwa safari ya kuwauguza wagonjwa wa saratani inawasukuma jamaa zao kwenye ufukara kwani wanalazimika kutumia kila walicho nacho kufanikisha matibabu.
Hii ni kwasababu, idadi ya wakenya walio na bima ya afya ya kitaifa NHIF ni asilimia 20 pekee. Elly Ochola ni msaidizi wa mamake ambaye anaugua saratani ya koo iliyo katika daraja la tatu. Amelazimika kutumia kila alicho nacho kumtibu mzazi wake wa kike kwani nduguze hawana ajira au hawako vizuri kifedha.
Kwa upande wa pili bima ya afya ya kitaifa ya NHIF inagharamia sehemu tu ya mahitaji ya tiba kwa wagonjwa wanaougua kwa muda mrefu kama vile saratani. Suala jengine lililojitokeza ni kuwa wakenya wengi hawana uelewa juu ya umuhimu wa kupimwa mapema hasa kwenye saratani zinazowaathiri zaidi wanawake kama ile ya shingo ya kizazi.
Asilimia 22 pekee ya walio masikini ndio wanaolifahamu hilo ikilinganishwa na asilimia 61 ya walio na uwezo kifedha zinaashiria takwimu za ripoti hiyo mpya. Idadi ndogo zaidi ya wanawake tayari wamepokea vipimo vya saratani ya shingo ya kizazi. Takwimu rasmi zinaonyesha kuwa watu alfu 47 wapya wanagunduliwa kuwa na saratani kila mwaka huku wengine alfu 35 wakifariki kwa ugonjwa huo kila mwaka.Kwa sasa vipo vituo vitatu pekee vya umma vya kutoa huduma za tiba ya mionzi kote nchini na mashine moja inagharimu shilingi nusu milioni.Tiba ya saratani inaweza kufikia hadi shilingi milioni moja za kenya.