FC Cologne yafufua matumaini kubakia Bundesliga
22 Januari 2018Mchezo wa 19 wa Bundesliga umeleta zaidi mvuto katika eneo la mkiani mwa msimamo wa ligi, ambapo Hamburg SV ambayo iko katika nafasi ya 17 ikiwa nyumbani iliikaribisha FC Cologne ambayo wengi wanaitabiria kuwa imo njiani kuelekea katika daraja la pili baada ya kuwa na pointi 9 tu kabla ya mchezo wa jioni ya Jumamosi. FC Cologne ilihitaji ushindi kwa kila hali ili kujiweka katika nafasi nzuri ya kupambana kujitoa kutoka katika hatari ya kushuka daraja. Na ndivyo walivyofanya dhidi ya Hamburg SV , kwa ushindi wa mabao 2-0.
Baada ya ushindi huo nahodha wa FC Cologne Matthias Lehmann alisema.
„Tumeshinda hadi sasa michezo mitatu mfululizo. Hakuna aliyeweza kuamini. Ukishindwa dhidi ya timu ya mwisho, kama ilivyo kwa Hamburg leo, morali inashuka. Kwetu sisi morali iko juu. Ndio sababu tunataka kuibeba hali hiyo katika mchezo wa wiki ijayo."
Hamburg imetengana na kocha wake Markus Gisdol na tayari wamemteua mchezaji wao wa zamani Bernd Hollerbach kuwa kocha wa timu hiyo.
Werder Bremen ambayo nayo imo katika eneo la hatari ya kushuka daraja , ikiwa nafasi moja tu juu ya Hamburg SV katika nafasi ya 16 na ikiwa na pointi 16 , moja tu zaidi ya Hamburg , ilipigana kiume dhidi ya mabingwa watetezi na mabingwa watarajiwa Bayern Munich na kukubali kipigo cha mabao 4-2 hali ambayo haitoi matumaini makubwa kwa Bremen kubakia pia katika daraja la kwanza. Hata hivyo mshambuliaji wa Bayern Thomas Mueller alikiri kwamba mchezo huo haukuwa rahisi kwa mabingwa hao.
„Leo haikuwa siku yetu nzuri, ambapo mambo yalikuwa yanakwenda tu. Mwanzoni tulikuwa kidogo wavivu. Bremen walifanya vizuri sana, katikati walifunga njia zote. Tuliwaruhusu Bremen kutumia mbinu zao na kutushambulia kwa urahisi kabisa. Lakini mwishoni tuliweza baadae kuchukua hatamu za mchezo huo."
Bayer yachupa
Bayer Leverkusen baada ya kipigo cha mabao 3-1 dhidi ya mabingwa Bayern Munich katika mchezo wa 18 wa Bundesliga, ilizinduka mara hii katika mchezo wa 19 na kuivuruga Hoffenheim siku ya Jumamosi kwa kuishindilia mabao 4-1 nyumbani. Bayer Leverkusen imechupa toka nafasi ya tano wiki iliyopita hadi nafasi ya pili ya msimamo wa ligi kwa kuwa na pointi 31, ikiwa ni pointi 16 nyuma ya viongozi wa ligi hiyo Bayern Munich. Kocha wa Leverkusen Heiko Herrlich hata hivyo alisema mchezo huo haukuwa rahisi kama matokeo yanavyoonesha.
„Iwapo kabla ya mchezo mtu angesema tungetoka na pointi moja, ningekubali haraka sana. Hoffenheim ni timu ngumu sana. Nafikiri leo tumecheza vizuri sana . Nimefurahi sana kupata pointi tatu."
FC Schalke 04 imefanikiwa kutoka suluhu jana Jumapili dhidi ya Hannover 96 kwa kufungana bao 1-1, lakini mchezo huo uligubikwa na hali ya mashabiki wa Schalke kupiga miluzi uwanjani wakimshutumu mchezaji wao wa kati Leon Goretzka kutangaza kwamba anahamia katika klabu ya Bayern Munich msimu ujao.
Hasira za mashabiki wa Schalke ni pamoja na kujivuta kwa Leon Goretzka kutangaza na mapema nia yake hiyo na hatimaye kuinyima mapato klabu ya Schalke , baada ya kutangaza nia hiyo akiwa mkataba wake unafikia mwisho na kuwa mchezaji huru na kwa hiyo kuondoka bila Bayern kulipa chochote kwa Schalke. Hata hivyo Goretzka amesema anatambua hisia za mashabiki wa Schalke.
„Sihitaji kumdanganya mtu na hata kujidanganya mimi binafsi. Ilikuwa ni hali tofauti kabisa, bila shaka. Kwamba timu haikuvurugika, na nimefurahi sana. Kwamba mashabiki wengi wameonesha kutoridhishwa kwa kupiga miluzi ni kitu kinachoeleweka na kwa kuwa kila kitu kilikuwa ndani ya mipaka yake, na ndivyo ilivyokuwa, kwa hiyo kila kitu kilikuwa sawa."
Dortmund yaporomoka
Borussia Dortmund imeporomoka hadi nafasi ya 6 kutoka nafasi ya tatu baada ya kutoka sare ya pili mfululizo siku ya Ijumaa dhidi ya Hertha Berlin. RB Leipzig ilipokea kipigo cha mabao 2-1 dhidi ya Freiburg na kuporomoka hadi nafasi ya 4.
Sakata la mvutano uliojitokeza kati ya Borussia Dortmund na mshambuliaji wake nyota Pierre-Emerick Aubameyang kutaka kuhamia klabu nyingine linaendelea. Mara hii lakini wahusika kutoka klabu ya Arsenal wamewasili mjini Dortmund kufanya mazungumzo ya siri na viongozi wa klabu hiyo ili kukamilisha uhamisho wa mchezaji huyo ambaye anaonekana hana hamu tena kucheza katika kikosi hicho cha BVB.
Kwa upande mwingine Alexis Sanchez wa Arsenal anaripotiwa kuwa atakuwa mchezaji wa Manchester United kuanzia leo baada ya kutolewa picha inayomuonesha mchezaji huyo kutoka Chile akiwa katika uwanja wa Old Trafford akivalia jezi ya klabu hiyo.
Sanchez , mwenye umri wa miaka 29 , anatarajiwa kuwa mchezaji wa Man United ambaye analipwa mshahara mkubwa zaidi kuliko wote , ambapo mshahara wake unakadiriwa kufikia zaidi ya pauni za Uingereza 500,000 kwa wiki.
Kocha wa Arsenal Arsene Wenger na Jose Mourinho wa Manchester United wamesema wanatarajia makubaliano ya pande mbili baina ya vilabu hivyo vya Premier League yatafanikiwa.
Wakati huo huo Henrick Mikhtariyan amekamilisha uhamisho wake kutoka Manchester United kwenda Arsenal. Mikhitariyan anaondoka Manchester United baada ya kushindwa kupata namba ya kudumu katika kikosi cha Jose Mourinho.
Mwandishi : Sekione Kitojo / ape / rtre / dpae
Mhariri: Iddi Ssessanga