Frank Habineza- sauti adimu ya ukosoaji Rwanda
1 Agosti 2017Frank Habineza anagombea kiti cha urais kwa mara ya kwanza baada ya miaka minane ya mapambano kuweza kukiandikisha chama chake na kupata nafasi ya kuingizwa katika makaratasi ya kupigia kura.
Frank Habineza ni mwanaharakati wa kulinda mazingira anayewania kuwa rais wa Rwanda. Habineza mwenye umri wa miaka 40 kiongozi wa chama cha Green Party amekabiliana na vitisho vya kuuwawa na ameshuhudia waungaji wake mkono wakipigwa, wakifungwa jela na kulazimishwa kuikimbia nchini hiyo na kwenda kuishi uhamishoni katika wakati akijaribu kuingia katika uwanja wa kisiasa nchini rwanda ambao una udhibiti mkubwa.
"Imekuwa ni safari ngumu , na pia safari ya hatari," ameliambia shirika la habari la Ufaransa AFP katika mahojiano katika ofisi yake katika mji mkuu Kigali, ambako walinzi wake wanalinda doria.
Alizaliwa uhamishoni nchini Uganda , baba yake akiwa ni Mhutu na mama yake Mtutsi, alirejea nchini Rwanda na kusomea masuala ya utawala. Pia alianza kuwa mwanaharakati wa asasi za kijamii , akifanya kampeni ya ulinzi wa mazingira.
Habineza alikuwa mwanachama wa chama btawala cha Rwandan Patriotic Front RPF lakini alijitoa na kujiunga na siasa za upinzani mwaka 2009 ili kuweza kuwa na chama mbadala kwa chama tawala ambacho kinatawala kwa mkono wa chuma.
Mkono wa chuma
Rais Paul Kagame amekuwa akishutumiwa kwa kuzuwia uhuru wa kutoa mawazo na kuzuwia vyama vya upinzani. Mbali na chama cha Habineza cha Green Party , vyama vyote vya upinzani vilivyosajiliwa vinamuunga mkono Kagame.
"Tulipoanzisha chama tulipigwa katika baadhi ya mikutano yetu na watu ambao walikuwa na silaha, watu waliwekwa korokoroni, walifungwa , wengine walikimbilia uhamishoni," amesema Habineza.
Chama chake kilizuiliwa usajili kabla ya uchaguzi wa mwaka 2010, na muda mfupi kabla ya uchaguzi mwili wa makamu wa rais wa chama cha Green Andre Rwisereka ulipatikana ukiwa umeharibika kabisa.
Habineza , ambae anasema binafsi pia alipokea vitisho vya kuuwawa , aliamua kukimbilia Sweden mwezi mmoja baadaye ambako familia yake hatimaye ilipata uraia.
Upinzani wabinywa Rwanda
Mwaka 2012 aliamua kurejea nchini Rwanda. Amesema kumuacha mkewe na watoto , ikiwa ni pamoja na mtoto wake wa kiume wa mwaka mmoja, ilikuwa kitu kigumu sana ambacho amewahi kufanya.
Chama chake hatimaye kilifanikiwa kusajiliwa mwaka 2013, mwezi mmoja tu kabla ya uchaguzi wa bunge, ambapo Habineza aliamua kutoshiriki kutokana na ukosefu wa muda wa matayarisho.
Mwaka 2015 alikuwa mgombea pekee kushiriki katika kura ya maoni ya mageuzi ya katiba inayomruhusu Kagame kuwania muhula wa tatu madarakani. Habineza alirejesha uraia wa Sweden ili kuweza kushiriki katika uchaguzi wa mwaka huu 2017 na ameendelea kukabiliana na vikwazo chungu nzima katika kila hatua.
Mwaka 2016 aliotolewa kutoka katika jengo la ofisi yake na nyumbani kwake bila kupewa taarifa , na kufanya kampeni pia imekuwa taabu kwake.
Mwandishi: Sekione Kitojo / afp
Mhariri: Mohammed Khelef