Merkel atoa wito wa mshikamano wa kimataifa dhidi ya corona
22 Novemba 2020Kansela wa Ujerumani Angela Merkel amewahimiza viongozi wa nchi za G20 kuendelea kushirikiana katika vita dhidi ya virusi vya corona, akiuambia mkutano wa kilele unaofanyika kwa njia ya video kuwa mengi yanastahili kufanywa ili kulidhibiti janga hilo.
Merkel aliyasema hayo wakati wa mkutano ulioandaliwa na Saudi Arabia na wakuu wa nchi na serikali kutoka madola yenye nguvu za kiuchumi duniani.
Soma pia: Mkutano wa G20 waanza chini ya kiwingu cha janga la COVID-19
"Tukisimama pamoja duniani, tunaweza kudhibiti na kukishinda kirusi hiki na madhara yake. Kwa hiyo juhudi zaidi inafaa.” Alisema katika ujumbe wa video.
Merkel amesema hii ni changamoto ya ulimwengu ambayo inaweza tu kukabiliwa kwa kushirikiana na mashirika ya kimataifa kama vile Shirika la Afya Ulimwenguni – WHO, Umoja wa Mataifa na G20, akiongeza kuwa viongozi wanahitaji kutoa fedha zaidi kuyasaidia mataifa maskini kupata chanjo.
Maneno yake yaliungwa mkono na Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron, ambaye pia aliwahutubia viongozi.
"Tunakabiliwa na mgogoro wa kiafya unaotishia maisha ya mamilioni ya watu,” Alisema Macron. "Lakini hapawezi kuwa na jibu mwafaka kwa janga hilo kama sio la kimataifa, lililoratibiwa na linalotokana na mshikamano.”
Mkutano huo wa kilele unaandaliwa kwa njia ya video na wenyeji Saudi Arabia kutokana na janga la corona.
Soma pia: G20 yarefusha muda wa mataifa maskini kulipa madeni
Mada kuu ni kuhusu ununuzi na usambazaji duniani, wa chanjo, madawa na vipimo kwa nchi za kipato cha chini ambazo haziwezi kumudu zenyewe gharama za aina hiyo.
‘Ufufuaji wa uchumi'
Wakati huo huo, Waziri wa Fedha wa Saudi Arabia Mohammed al-Jadaan amesema mkutano huo "utalenga kuimarisha ushirikiano wa kimataifa kuunga mkono ufufuaji uchumi wa ulimwengu.”
Soma pia: Saudi Arabia mwenyeji wa mkutano wa mataifa ya G20
"G20 iliahidi mwezi Machi kufanya kinachowezakana kulidhibiti janga hili na kuyalinda maisha ya watu,” Amesema Waziri Mkuu wa Uingereza katika taarifa. "Lazima tuhakikishe tunaitekeleza ahadi hiyo.”
Hata hivyo, viongozi wa G20 wanakabiliwa na ongezeko la shinikizo la kusaidia kuyafuta madeni yote katika mataifa yanayoendelea.
Kupambana na mabadiliko ya tabia nchi
Suala la mabadiliko ya tabia nchi pia linatarajiwa pia kuwa mada kuu, huku mabadiliko ya uongozi wa Marekani yakiongeza matumaini ya juhudi za pamoja zaidi katika kiwango cha G20 za kupambana na ongezeko la joto duniani.
Soma pia: G20 yasema ni muhimu kudhibiti covid ili kusaidia uchumi
Chini ya Rais Donald Trump, Marekani ilijiondoa katika makubaliano ya Paris ya kupambana na mabadiliko ya tabia nchi, lakini uamuzi huo huenda ukabatilishwa na Rais mteule Joe Biden.
jf/aw (AFP, Reuters)