G7 kuachana na makaa ya mawe ifikapo 2035
30 Aprili 2024Haya yamesemwa jana na maafisa wa Uingereza na Italia katika uamuzi uliothibitishwa jioni ya Jumatatu (Aprili 29) na wizara ya masuala ya kiuchumi ya Ujerumani.
Msemaji wa wizara hiyo amesema kuwa nchi hiyo ilitekeleza jukumu muhimu katika uamuzi wa kuweka wazi tarehe ya mwisho ya uzalishaji wa umeme kwa kutumia makaa ya mawe kwa nchi zote za G7.
Soma zaidi: Nchi tajiri zatumia mabilioni kuendeleza sekta ya nishati asilia
Awali, Waziri wa Nishati wa Uingereza Andrew Bowie alikuwa ametangaza makubaliano hayo, akiliambia shirika la habari la CNBC pembezoni mwa mkutano huo wa mawaziri wa G7 kwamba wamekubaliana kuacha matumizi ya makaa ya mawe katika nusu ya kwanza ya miaka ya 2030.
"Haya ni makubaliano ya kihistoria ambayo hayakuweza kufikiwa wakati wa mkutano wa mwaka jana wa COP 28 mjini Dubai," alisema.
Mawaziri hao wa G7 walitarajiwa kutoa tamko la mwisho siku ya Jumanne (Aprili 30).