Gavana Mike Sonko akanusha mashtaka ya ufisadi dhidi yake
9 Desemba 2019Gavana wa Nairobi nchini Kenya Mike Mbuvi Sonko amesema hana hatia dhidi ya mashataka zaidi ya 30 ikiwemo utakatishaji pesa, kupokea rushwa na kutumia madaraka vibaya kwa maslahi binafsi baada ya kufikishwa mahakamani chini ya ulinzi mkali hii leo.
Mike Sonko ni kiongozi wa ngazi ya juu wa hivi karibuni kukamatwa kuhusiana na mashataka yanayohusiana na rushwa nchini Kenya na anatuhumiwa kujifaidisha kutokana na manunuzi ya kiholela na kutowa malipo ya dola milioni 3.5.
Mbele ya jaji Douglas Ogoti katika mahakama ya kupambana na rushwa, amekanusha kuwa na hatia katika mashtaka yote yanaomkabili.
Mwendesha mashtaka wa serikali alitowa ufafanuzi zaidi kuhusu akaunti za benki za Gavana Sonko na tarehe mbalimbali ambapo fedha zilionekana kuingia kutoka kwa wakandarasi waliopata zabuni za Kaunti hiyo.
Sonko amekaa kizuizini mwishoni mwa juma baada ya kukamatwa mjini Voi katika hatua iliyoshuhudia vurugu akipambana na polisi kabla ya kuingizwa kwenye helikopta na kusafirishwa hadi Nairobi.