Ghasia zazuka uchaguzi mkuu Madagascar
25 Oktoba 2013Ghasia hizo pia zimesababisha kifo cha afisa wa serikali, huku kituo kimoja cha kupigia kura kikivamiwa na kingine kuchomwa moto.
Vurugu hizo zimesababisha kifo cha kiongozi mmoja wa wilaya aliyeuawa katika kituo cha kupigia kura, Mashariki mwa mji wa Benenitra.
Taarifa hiyo imetolewa na ofisi ya mambo ya ndani ya nchi hiyo kwa shirika la habari la AFP, bila kutoa maelezo ya kina.
Mbali ya mauaji hayo, mtu mmoja pia ameripotiwa kutekwa nyara kutoka kwenye kituo cha kupigia kura, eneo la Bezaha pia mashariki mwa nchi hiyo, wakati kituo kingine cha kupigia kura kilichopo kaskazini mwa wilaya ya Tsaratanana, kikichomwa moto.
Hali hiyo ilisababisha kusimamishwa kwa zoezi la kupiga kura hadi hapo vituo hivyo vitatu vya kupigia kura vilipohamishwa mahali pengine, huku katika maeneo mengine, uchaguzi huo ukiwa unaendelea salama.
Awali alipohojiwa, mwangalizi wa uchaguzi kutoka shirika la Umoja wa Mataifa, Maria Muniz de Urquiza alikaririwa akisema kuwa hakukuwa na tatizo kubwa katika zoezi zima la kupiga kura.
Kasi ya wapiga kura iliongezeka mchana baada ya zoezi hilo kuanza taratibu, wakati ambapo wapiga kura waliamua kuendelea na majukumu yao ya kila siku
Wapiga kura wamefuata taratibu zote
Rais wa zamani wa Msumbiji, Joachim Chissano ambaye ni mpatanishi kutoka Nchi za Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika, SADC, katika mgogoro wa Madagascar ambaye yupo nchini humo, amesema vituo vingine alivyovitembelea wapiga kura waliendelea salama na zoezi la kupiga kura, huku wengi wa wapiga kura wakiwa wanafahamu taratibu zote za kupiga kura.
Kwa upande wake kiongozi wa kamisheni ya uchaguzi nchini humo, Beatrice Atallah ameiambia radio ya taifa nchini humo kuwa katika baadhi ya vituo vya kupigia kura, wapiga kura wameongezeka kufikia asilimia 50, ingawa wengine wameshindwa kupiga kura kutokana na kukosa vitambulisho vya kupigia kura, huku wengine majina yao yakikosekana kwenye orodha ya wapiga kura
Vurugu hizo zinakuja huku wapiga kura wakitarajia kwamba uchaguzi huo ungekuwa ni mwanzo wa kudumisha amani ili kuleta matumaini ya kisiasa, tangu kutokea kwa mgongano kisiasa mwaka 2009, na kuungwa mkono na rais Chissano ambaye amesema, raia wa Madagascar wanatarajia kuona nchi hiyo ikifurahia matunda ya amani na kuwa na serikali inayoheshimika duniani na kuwa mfano wa kuigwa.
Watu milioni 7.8 wajiandikisha kupiga kura
Tume ya Taifa ya uchaguzi nchini humo imetangaza kuwa zaidi ya watu milioni 7.8 wenye haki ya kupiga kura wamejiandikisha kupiga kura katika vituo milioni 20,000 vya kupigia kura
Jumla ya wagombea 33 wanapigiwa kura katika kiti cha urais wakiwemo mawaziri wa zamani wa nchi hiyo , wanadiplomasia, wachambuzi wa siasa na wasanii, ingawa ni wagombea sita tu wenye dalili za kushinda.
Uchaguzi huo unaleta matumaini kwa raia wa Madagascar kuwa utakuwa ni mwanzo mpya baada ya miaka minne ya kususiwa misaada na uwekezaji na kuyumbisha uchumi wa nchi hiyo ulioambatana na kuongezeka kwa umaskini
Mwandishi. Flora Nzema/APE/RTRE/AFPE
Mhariri: Suamu Yusuph Mwasimba