Guinea Bissau kufanya raundi ya pili ya uchagauzi Aprili
22 Machi 2012Kwa mujibu wa Tume ya taifa ya uchaguzi, ya Guinea Bissau Waziri Mkuu Carlos Gomes aliongoza katika raundi ya kwanza ya uchaguzi wa Rais. Lakini hakupata kura za kutosha ili kuweza kushinda moja kwa moja. Sasa Waziri Mkuu Gomes atapambana na aliekuwa Rais wa Guinea Bissau Kumba Lala katika raundi ya pili.
Kwa mujibu wa matokea ya awali yaliyotangazwa na tume ya uchaguzi, Waziri Mkuu Carlos Gomes Junior amepata asilimia 48. 97 ya kura na mpinzani wake mkuu, aliyekuwa Rais Dr Kumba Lala amepata asilimia 23. 36. Madhali hakuna aliefikia asilimia 50 ya kura, raundi ya pili itafanyika tarehe 22 mwezi ujao.
Juu ya uchaguzi huo Waziri Mkuu Carlos Gomes Junior amesema,"anatetea sera ya mdahalo wa kudumu kati ya vyombo vyote vya dola, kama vile baina ya bunge na serikali, ili kudumisha utulivu nchini na kuendeleza ustawi."
Katika uchaguzi huo Waziri Mkuu Carlos Gomes Junior alisimama kwa niaba ya chama cha uhuru wa Guinea na visiwa vya Cape Verde PAIGC ambacho hapo awali kilikuwa cha ukombozi. Bwana Carlos amesema ameridhishwa na matokea ya raundi ya kwanza na amekanusha madai ya wizi wa kura. Bwana Gomes ameeleza kuwa hapendelei sana kufanyika raundi ya pili ya uchaguzi lakini amesema katika demokrasia mtu anapaswa kuyakubali matakwa ya wananchi.
Mpinzani wake Mkuu,Rais wa hapo awali Dr. Kumba Yala aliongoza mwito wa viongozi watano wa upinzani wa kutaka matokeo ya uchaguzi uliofanyika jumapili iliyopita yabatilishwe .Dr Kumba amedai kwamba udanganyifu ulifanyika .
Lakini watazamaji kutoka Umoja wa Afrika,Jumuiya ya uchumi ya nchi za Afrika Magharibi na kutoka nchi zinazotumia lugha ya kireno wamesema kuwa uchaguzi wa jumapili ulikuwa huru na wa haki.
Mwandishi:Johannes Beck
Tafsiri:Mtullya abdu
Mhariri:Josephat Charo..