Guru ahukumiwa kifungo India
28 Agosti 2017Lakini amri ya kumfyatulia risasi mtu yeyote na kumuua, kutotembea usiku na polisi wengi kuwekwa katika eneo hilo kuliwazuwia waandamanaji kufanya ghasia zaidi baada ya hukumu hiyo.
Mamia kwa maelfu ya polisi waliimarisha usalama na kulifunga eneo kubwa la jimbo la kaskazini la Haryana na Punjab ambako Gurmeet Ram Rahim Singh, mwenye umri wa miaka 50 , ana wafuasi wengi.
Polisi katika jimbo la Haryana wametoa amri kupiga risasi waandamanaji wanapowaona kabla ya kutolewa hukumu na polisi imeamuru kesi hiyo kufanyika nje ya jela ambako Singh anashikiliwa.
Mamia ya wafuasi walifanya ghasia wakati alipohukumiwa siku ya Ijumaa, wakishambulia vituo vya treni, mabasi na magari ya televisheni.
Kiasi watu 38 waliuwawa na zaidi ya 200 walijeruhiwa , na kusababisha ukosoaji kwamba chama tawala cha waziri mkuu Narendra Modi , ambacho pia kinatawala katika jimbo la Haryana , ama hakina uwezo ama hakitaki kuchukua hatua dhidi ya wafuasi wa Singh.
Singh ashutumiwa kwa ubakaji
"Mahakama imeamuru mshitakiwa afungwe miaka 10 jela," Ram Niwas , mtaalamu anayehusika na masuala ya sheria na utulivu katika jimbo la Haryana , ameliambia shirika la habari la Reuters.
Kesi hiyo ni ya tangu mwaka 2002 wakati wanawake wawili wafuasi wake walipomshutumu Singh kwa ubakaji katika makao makuu ya jumuiya yake ya Dera Sacha sauda katika mji wa Sirsa.
Singh , ambaye pia anafahamika kama guru wa vito vya thamani na nguo , kutokana na nguo na vito anavyovaa katika filamu anazozitayarisha mwenyewe, anakabiliwa na kifungo cha miaka saba chini ya sheria mpya ngumu za ubakaji.
Wakili wa Singh , A.K. Panth , amesema mteja wake hana hatia na atakata rufaa. Vipassana Insaan , msemaji wa Dera sacha sauda , amewataka wafuasia wa Singh kuheshimu amri ya mahakama.
"Mapambano yetu ya kisheria hayatamalizika hapa. Mteja wetu hana hatia kabisa," amesema Panth.
Aahidi kukata rufaa
Vituo vya televisheni nchini India vimeripoti kwamba Singh alifadhaika sana baada ya hukumu kupitishwa na kukataa kusogea na kutoka nje ya chumba cha mahakama, akisema hana hatia.
Jela katika mji wa Rohtak , kilometa 66 kutoka New Delhi, iligeuzwa kuwa ngome, ambapo waandishi habari waliopigwa marufuku kukaribia eneo hilo kwa umbali wa kilometa 1.6 na barabara ziliwekwa uzio wa waya.
V. Umashankar , kamishna maalum katika jimbo la Haryana , amesema marufuku ya kutembea ovyo inaendelea katika mji wa Sirsa na maeneo ya Rohtak.
Kuhukumiwa kwa Singh katika kesi ya ubakaji ni ya hivi karibuni katika mlolongo wa kesi zinazohusisha viongozi wa kiroho ambao wamekuwa wakishutumiwa kwa kuwadhalilisha kingono wafuasi wao, wakijilimbikia fedha ambazo hazotozwi kodi na kupata ushawishi wa wanasiasa.
Mwandishi: Sekione Kitojo / rtre
Mhariri: Mohammed Abdul Rahman