1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Atakumbukwa milele na jamii

14 Aprili 2015

Kifo cha mwandishi vitabu Günter Grass,na uamuzi wa waziri wa zamani wa mambo ya nchi za nje wa Marekani Hillary Clinton kugombea kiti cha rais ni miongoni mwa mada zilizochambuliwa zaidi magazetini.

https://p.dw.com/p/1F7Wf
Günter GrassPicha: picture-alliance/dpa/Gambarini

Tunaanzia lakini Lübeck ambako habari za kufariki dunia mwandishi vitabu mashuhuri nchini Ujerumani,mshindi wa tuzo ya Nobel ya uandishi fasaha,Günter Grass zimeuhuzunisha ulimwengu wa kisiasa,kitamaduni na kijamii.Gazeti la "Landeszeitung" linaandika:"Günter Grass ni miongoni mwa waandishi mashuhuri wachache kabisa wa Ujerumani ambae kila mmoja anahisi anamjua.Tamthilia zake tatu;"Blechtrommel" au Goma la bati","Katz und Maus" au Paka na panya na "Hundejahre" au miaka ya sulubu zimempandisha Grass,katika miaka ya 60,nafasi ya juu kabisa ya waandishi fasaha wa baada ya enzi za vita nchini Ujerumani.Kazi aliyokuwa akiifanya kwa usumbufu kwa miongo kadhaa haikuingia katika enzi ya zamani ya ufanisi,haikugusa nyonyo za watu.Mivutano ya hadharani mfano ule pamoja na Marcel Reich-Ranicki,kukawia kwake kuungama kwamba aliwahi kutumikia kikosi cha SS wakati wa utawala wa wanazi au hata shairi lake la mwaka 2012 lililoikosoa Israel,yote hayo yamezusha mijadala moto moto humu nchini.Kitakachosalia ni tamthilia aliyoitunga akikumbuka mji alikozaliwa wa Gdansk.Oskar Matzerath ataendelea kupiga goma.

Ujerumani itamkumbuka daima Günter Grass

Gazeti la "Neue Osnabrücker linahisi kifo cha Günter Grass kinaacha pengo katika jamii.Gazeti linaendelea kuandika:"Kwa kuiaga dunia,inatoweka pia nuru iliyomulika na kuipa sura jamii nzima.Grass ni miongoni mwa wale waliokuwa wakijiamini,na kudai marekebisho.Upande huo kila mtu alikuwa akimhusudu hata wale ambao hawakuwa na maoni sawa na yake.Tangu sasa imeshaanza kudhihirika,sauti ya nguvu ya Grass itakumbukwa daima.Grass watu walikuwa wakimuona.Na pengine hiyo ndio sifa maalum ya enzi hizi za digitali.Ujerumani bila ya Günter Grass,kwa kweli hakuna anaeamini.

Günter Grass und SPD-Vorsitzender Willy Brandt 1976
Günter Grass pamoja na kansela wa Zamani Willy Brandt mnamo mwaka 1976Picha: picture-alliance/dpa/D. Klar

Hillary Clinton apigania wadhifa wa rais wa Marekani

Mada nyegine iliyochambuliwa zaidi na wahariri wa magazeti ya Ujerumani leo hii inahusiana na uamuzi wa waziri wa zamani wa mambo ya nchi za nje wa Marekani bibi Hillary Clinton kugombea wadhifa wa rais nchini mwake na jinsi tangazo hilo lilivyomfanya waziri wa mambo ya nchi za nje wa Ujerumani kuvunja miko.Gazeti la "Lausitzer Rundschau linaandika:"Ni desturi za muda mrefu katika nchi kumuona waziri kutoingilia mjadala unaohusiana na kuteuliwa kwa njia za kidemokrasia waziri mwenzake .Na pengine Frank-Walter Steinmeier ni waziri wa Ujerumani anaeshika sana miko hiyo-na hasemi kitu bila ya kukipima mara mbili.Ndio maana mtu ameshangaa alipozungumzia kinaga ubaga kupitia gazeti moja kuhusu nafasi ya Hillary Clinton hata kabla ya mwenyewe kutangaza atapigania wadhifa wa rais.Ndo kusema hali hiyo imesababishwa na furaha kutokana na ushirikiano wa muda mrefu wa zamani pamoja na mtu anaemthamini.Labda.Lakini kwa vyovyote vile lilikuwa kosa bayana.

Hillary Clinton
Mgombea kiti cha rais wa Marekani,Hillary Clinton wa chama cha DemocraticPicha: Kamm/AFP/Getty Images

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/Inlandspresse

Mhariri . Mohammed Abdul-rahman