Ripoti nyingine yaituhumu Burundi kuvunja haki za binadamu
29 Januari 2020Kundi hilo la kujitegemea lijulikanalo kama Burundi Human Rights Initiative, au Mpango wa haki za Binadamu nchini Burundi, BHRI limechapisha ripoti mpya yenye kichwa kisemacho, ''Amani bandia katika nchi ya hofu: Kilicho nyuma ya mgogoro wa haki za binadamu nchini Burundi''.
Ripoti hiyo inasema ukipinga serikali nchini Burundi maisha yako yako hatarini. Inawanukuu maafisa wa chama tawala cha CNDD/FDD kusema kwamba polisi waliovalia sare za jeshi husindikiza magari yaliyopakia miili ya watu waliouawa, ikipelekwa katika makaburi ambayo yamewekwa tayari.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo, maafisa walionukuliwa walisema mbinu hiyo inafanywa makusudi ili kuficha mauaji hayo yasione na mashirika ya kutetea haki za binadamu, katika juhudi za kuihadaa jumuiya ya kimataifa kuwa hali ni ya utulivu mnamo kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi mkuu.
Vijana wa Imbonerakure watajwa tena
Ripoti hii ya BHRI inakuja wiki chache baada ya nyingine iliyotolewa na shirika la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch, ambayo iliwashutumu vijana wa chama tawala wajulikanao kama Imbonerakure, kuendesha vitendo vya mauaji, ubakaji, kuwashika watu mateka na kuwatisha watu wanaoshukiwa kuwa wapinzani wa kisiasa.
Shirika la habari la DPAE limesema limejaribu kupata majibu ya waziri wa haki za binadamu wa Burundi Martin Nivyabandi bila mafanikio.
Ingawa mara kwa mara serikali mjini Bujumbura imekanusha tuhuma hizi dhidi yake, maafisa wa Human Rights Watch na pia Umoja wa Mataifa wamesema wamepata ushahidi wa ukiukwaji wa haki za binadamu, hata baada ya kumalizika kwa vita vya webyewe kwa wenyewe mwaka 2005.
Wingu la hofu
Ripoti ya Umoja wa Mataifa iliyochapishwa mwaka uliopita ilisema watu wa Burundi walikuwa wakiishi chini ya wingu la hofu, kukiwa na dalili kuwa matatizo makubwa yanaweza kutokea kabla ya uchaguzi unaokaribia.
Kundi la haki za binadamu la BHRI limesema katika ripoti yake ukweli kwamba maiti ambazo hazitambuliwi zinaendelea kugunduliwa katika mikoa mbali mbali ya Burundi mwaka huu wa 2020 ni hali ya kutia wasiwasi.
Ripoti hiyo inasema wengi wa wahanga wa unyanyasaji nchini Burundi ni wafuasi wa chama cha upinzani chaCNL, ambacho kiongozi wake ni mpinzani mkuu wa rais wa Burundi Pierre Nkurunziza.
Makamu rais wa Burundi Gaston Sindimwo ameliambia shirika la habari la Associated Press kuwa madai yaliyomo katika ripoti hiyo ni uvumi uliozoeleka wenye lengo la kupandikiza hofu miongoni mwa raia.
dpae, ape