1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mashambulio ya maguruneti yashika kasi

22 Juni 2015

Ikisalia wiki moja kabla ya uchaguzi wa bunge na mikoa unaozusha mabishano nchini Burundi,watu wanne wameuliwa na zaidi ya 30 kujeruhiwa usiku wa jana kuamkia leo katika wimbi jipya la mashambulio ya maguruneti.

https://p.dw.com/p/1Flm1
Matumizi ya nguvu nchini BurundiPicha: AFP/Getty Images/C. de Souza

Ofisi ya rais wa Burundi inawatuhumu wapinzani wa rais Pierre Nkurunziza kuwa nyuma ya mashambulio hayo katika wakati ambapo wapinzani wao wanakanusha na kuilaumu serikali "kutaka kuyatumia mashambulio hayo ili kuwatokomeza wapinzani wake."

Matatu kati ya mashambulio manne yamelenga mikahawa mikoani.Shambulio baya kabisa-ambapo watu wanne wameuwawa na 25 kujeruhiwa limetokea Ngozi,katika mkoa wa kaskazini alikozaliwa rais Nkurunziza.Mashambulio mawili mengine yametokea karibu na hapo katika mji wa Kirundo ambako mtu mmoja amejeruhiwa na Muyinga ambako hakuna aliyejeruhiwa.Habari hizo zimetangazwa na magavana wa maeneo hayo.

Shambulio la nne lilipelekekea polisi wawili waliokuwa wakipiga doria kujeruhiwa mjini Bujumbura katika mtaa matata wa Musaga-kwa mujibu wa afisa mmoja wa ngazi ya juu wa polisi ambae hakutaka jina lake litajwe.

Mashambulio ya maguruneti

Katika wakati ambapo vuguvugu la malalamiko lililoanza April 26,baada ya rais Nkurunziza kutangaza azma ya kugombea mhula wa tatu madarakani,limeanza kupungua majiani,miripuko ya maguruneti imeongezeka katika wakati ambapo tarehe za uchaguzi wa bunge juni 29 ijayo na ule wa rais july 15 zinakurubia.

Deutschland Burundi Proteste gegen Präsident Nkurunziza in Köln
Maandamano dhidi ya mhula wa tatu wa rais NkurunzizaPicha: DW/B. Barry

Askari polisi 11 walijeruhiwa usiku wa ijumaa kuamkia jumamosi kufuatia mashambulio kadhaa ya maguruneti mjini Bujumbura na juni 18 iliyopita shambulio la guruneti likawajeruhi vibarua watatu waliokuwa wakifanya kazi katika kiwanda kimoja huko huko mjini Bujumbura.

Wakikosoa patashika ya kisiasa nchini Burundi,mawaziri wa mambo ya nchi za nje wa Umoja wa Ulaya wametishia hii leo na kwa mara ya kwanza kuwawekea vikwazo maalum viongozi wanaohusika na vitendo vya matumizi ya nguvu na unyanyasaji au wale "watakaokorofisha juhudi za kusaka ufumbuzi wa kisiasa."

Mazungumzo yamekwama kati ya kambi ya rais Nkurunziza na mahasimu wake,upande wa upinzani na mashirika ya kijamii wanaohisi kwamba katiba na makubaliano ya Arusha-yaliyofungua njia ya kumalizika vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyoangamiza maisha ya watu laki tatu kati ya mwaka 1993 na 2006-hayamruhusu rais Nkurunziza kugombea mhula mwengine.

Juhudi za kuyafufua mazungumzo ya amani

Ili kuyafufua mazungumzo hayo Umoja wa mataifa umemteua mjumbe maalum Abdoulaye Bathily wa Senegal aliyewasili Burundi jumapili hii.

nach Putschversuch - Präsident Pierre Nkurunziza zurück im Amt
Rais Pierre NkurunzizaPicha: Reuters/G. Tomasevic

"Mashambulio yote haya ya maguruneti yanahusiana na uchaguzi" amesema afisa mmoja wa ngazi ya juu wa polisi,akiwatuhumu "wapinzani wa mhula wa tazu" anaosema wanataka kuzuwia uchaguzi usiitishwe.

Afisa mmoja wa mawasiliano katika ofisi ya rais Willy Nyamitwe ameulaumu upande wa upinzani kutaka kuyarejea yaliyotokea mwaka 2010 waliposusia uchaguzi na matokeo yake yakawa kuzuka machafuko.

Lakini upande wa upinzani umelaani vikali mashambulio tofauti yaliyotokea."Vuguvugu letu ni la amani" amesema mbunge Jérémie MInani ambae ni msemaji wa kongamano linalowaleta pamoja wapinzani na mashirika ya kiraia.Haondoi uwezekano wa kuwepo mpango wa serikali kuzusha fujo na kuwatwika jukumu wapinzani ili baadae waweze kuwaandama wale wote wanaopinga mhula wa tatu wa rais Nkurunziza.

Maandamano dhidi ya mhula wa tatu wa rais Nkurunziza aliyekwisha chaguliwa mwaka 2005 na 2010 yameitumbukiza Burundi katika mzozo mkubwa wa kisiasa,uliogubikwa na machafuko yaliyoangamiza maisha ya watu wasiopungua 70-kwa mujibu wa shirika linalopigania haki za binaadam.

Licha ya shinikizo la jumuia ya kimataifa inayohisi masharti muhimu ya kuitishwa uchaguzi bado hayakutekelezwa nchini Burundi,serikali iliyokwisha badilisha tarehe za chaguzi hizo za bunge na rais,imeondowa uwezekano wa kuuakhirisha ikidai inabidi iheshimu ratiba yaani muda wa kumalizika kipindi cha bunge na mhula wa rais.

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/AFP

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman