1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
Janga

Hali ni ya kukata tamaa Haiti, UN yaambiwa

27 Septemba 2022

Maafisa wamelielezea baraza la usalama la UN juu ya janga la kibinadamu nchini Haiti jana, huku taifa hilo likizidi kukosa matumaini baada ya wiki kadhaa za vurugu na mashambulizi dhidi ya maghala ya chakula cha msaada.

https://p.dw.com/p/4HQ4t
Haiti, Port-au-Prince | Proteste gegen steigende Treibstoffpreise
Picha: Odelyn Joseph/AP/dpa/picture alliance

Maandamano na uporaji vimeitikisa nchi hiyo tangu Septemba 11, wakati waziri mkuu Ariel Henry alipotangaza kupandishwa kwa bei za mafuta, akisema ruzuku juu ya nishati hiyo zimekuwa ghali sana kwa taifa hilo ambalo ni mmoja ya maskini zaidi duniani.

Mjumbe wa Umoja wa Mataifa kwa ajili ya Haiti Helen La Lime, alisema wakati wa mkutano wa dharura la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa mjini New York, kwamba mzozo wa kiuchumi, mzozo wa magenge na mzozo wa kisiasa imekutana  na kusababisha janga la kibinadamu, na kuongeza kuwa kabla ya machafuko ya sasa ya kiraia, Wahaiti takribani milioni 4.9 walikuwa katika hali ya kuhitaji msaada wa kibinadamu.

USA | Abstimmung im UN-Sicherheitsrat über die Haiti-Resolution
Baraza la usalama la Umoja wa Mataifa likiwa kikaoni.Picha: Eskinder Debebe/UN Photo/Xinhua/IMAGO

"Hatupaswi kupteza matumaini bali kuunganisha juhudi zetu kutafuta njia ya mustakabali bora. Suluhisho linaloongozwa na Wahaiti ndiyo hatua ya kwanza muhimu kushughulikia mzozo wa sasa. Ili kuwasadia Wahaiti katika juhudi zao kuelekea mustakabali bora, baraza hili laazima lichukue hatua za haraka," alisema La Lime.

Katika muda wa wiki mbili zilizopita pekee, La Lime amesema mashambulizi dhidi ya shirika la mpango wa chakula duniani, WFP, yamesababisha hasara ya takribani tani 2,000 za chakula cha msaada kinachokadiriwa kuwa na thamani ya dola milioni 5, ambacho kingesaidia jumla ya hadi ya watu 200,000 wenye uhitaji zaidi nchini Haiti katika muda wa mwezi mmoja ujao.

Soma pia: Marekani yamshtaki aliehusika mauaji Rais Haiti

Alisema bohari ya mafuta mjini Verreux imekuwa katika hali ya mzingiro kwa zaidi ya wiki moja, ikizuwiwa na magenge ya wahalifu, huku uhaba wa mafuta ukiathiri uwezo wa taifa zima kufanya kazi, ikiwemo kufungwa kwa hospitali.

Waziri wa mambo ya nje wa Haiti Jean Victor Geneus, ambaye pia alihudhuria kikao hicho cha baraza la usalama, alisema mzingiro huo umesababisha pia eneo kubwa zaidi la viwanda nchini humo kusitisha kazi, na kupelekea upotevu wa nafasi 12,000 za ajira.

Alibanisha kuwa kampuni binafsi zinatishia kuondoka nchini humo na kwamba ufunguaji wa shule, ambao tayari umeahirishwa hadi Oktoba 3, umegeuka dhana zaidi kuliko uhalisia.

Haiti I Protest
Polisi wakimtia nguvuni mwanaume aliekamatwa akipora wakati wa maandamano ya kupinga kupanda kwa bei za mafuta mjini Port-au-Prince, Septemba 16, 2022.Picha: Odelyn Joseph/AP/picture alliance

Viwango vya kuvunja matumaini

Naibu Mkurugenzi wa WFP, Valerie Guarnieri alisema badala ya kupiga hatua mbele, hali ya sasa nchini Haiti kwa bahati mbaya imefikia viwango vipya vya kuvunja matumaini, na kuliambia baraza la usalama kwamba katika muda wa chini ya mwaka mmoja, bei ya chakula cha imepanda kwa asilimia 52.

Soma pia: Raia wa Haiti waelezea hasira zao kuhusiana na ukosefu wa msaada kutoka kwa serikali

Alisema wanataraji hali ya upatikanaji wa chakula kuzorota zaidi mwaka huu, na kupita rekodi ya watu milioni 4.5 waliokaridiriwa kukumbwa na hali ya mgogoro au mbaya zaidi ya ukosefu wa chakula, ikiwemo watu milioni 1.3 walioko katika dharura.

Mnamo mwezi Julai, Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lilipitisha azimio kuyaomba mataifa wanachama wa Umoja wa Mataifa kupiga marufuku uhamishaji silaha ndogondogo kwa magenge yanayoendesha shughuli zake nchini Haiti, bila hata hivyo kwenda mbali kulaazimisha utekelezaji wa marufuku hiyo kama ilivyotakiwa na China.