Hamas yafyatua zaidi ya maroketi 200 kuelekea Israel
12 Mei 2021Ndege ya kijeshi ya Israel imelishambulia jengo la ghorofa tisa katika mji wa Gaza na kulisambaratisha. Jengo hilo lilikuwa la makazi ya watu, makampuni za uzalishaji wa vifaa tiba na kliniki ya meno. Ndege hizo zilofyatua maroketi ya onyo kutokea kwenye ndege isiyo na rubani kuwatahadharisha watu kuhusu mashambulizi ya mabomu yaliyofuata, mapema Jumatano hii.
Hata hivyo hakukua na taarifa ya majeruhi ama vifo.
Kundi hilo lililojihami kwa silaha la Hamas, limesema kwenye taarifa yake kwamba pamoja na maroketi hayo 200, lilikuwa likijiandaa kufyatua makombora mengine 110 kuelekea mji wa Tel Aviv na 100 katika mji wa Beersheva, ili kulipiza kisasi cha mashambulizi yaliyoanzishwa na Israel kwenye makazi ya raia na jengo hilo la mjini Gaza.
Hayo yanafanyika wakati waziri mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu akitangaza hali ya dharura katika jiji la Lod, wakati polisi ikiwatuhumu wakazi wa Palestina kwa kusababisha kusambaa kwa machafuko.
Baraza la usalama la Umoja wa Mataifa, hii leo litafanya kikao cha dharura kuujadili mzozo huo, na mjumbe wa Mashariki ya Kati kwenye umoja huo Tor Wennesland anatarajiwa kuwaarifu wanachama kuhusiana na hali ilivyo. Kikao hicho cha ndani kimeitishwa na China, Tunisia na Norway.
China inshikilia uenyekiti wa kupokezana mwezi huu na ujumbe wake umethibitisha mipango ya mkutano wa pili wa dharura katika kipindi cha siku tatu. Hii ni ishara ya wasiwasi unaoongezeka katika jumuiya ya kimataifa kutokana na kusambaa kwa mzozo huo, pamoja na miito kwa Israel ya kusitisha mpango wake wa kuwahamisha raia.
Makabiliano ya karibuni kati ya Israel na Palestina yameibua hali ya wasiwasi na Israel imeashiria kwamba inaongeza kampeni zake za kijeshi.
Mashirika: AP