Hamas yatangaza usitishaji wa mapigano
27 Julai 2014Msemaji wa Hamas Sami Abu Zuhri amesema katika taarifa kwa kujibu ombi la Umoja wa Mataifa la kuingilia kati kwa kufuatilia hali hiyo makundi ya wapiganaji wamekubaliana kwamba usitishaji wa mapigano wa saa 24 uanze kuanzia saa nane mchana.
Zuhri amesema usitishaji huo wa mapigano utazingatiwa kabla ya siku tatu za mapumziko ya Siku Kuu ya Waislamu ya Eid al - Fitr ambayo huadhimisha kukamilika kwa mwezi mtukufu wa Ramadhan na inategemewa kuwa Jumatatu.
Mashambulizi mapya ya Israel
Usitishaji huo wa mapigano kwa misingi ya kibinaadamu umesambaratika huko Ukanda wa Gaza baada ya Israel Jumapili (27.07.2014) kuanza mashambulizi yake mapya kujibu mapigo ya maroketi yaliyovurumishwa kusini mwa Israel na wanamgambo wa Kipalestina.
Vifaru vya Israel na mizinga viliushambulia ukanda huo wa mwambao na kusababisha moshi mzito kufuka angani na kuashiria kumalizika kwa suluhu ya kusitisha mapigano ya saa 24 iliojiamuliwa yenyewe hapo awali.
Taarifa ya jeshi la Israel imesema katika taarifa kufuatia mashambulizi ya maroketi ya Hamas katika muda wote wa suluhu hiyo ambayo imezingatiwa kwa maslahi ya wananachi wa Gaza jeshi hivi sasa linaanzisha mashambulizi yake ya anga, majini na nchi kavu katika Ukanda wa Gaza.
Muda mfupi baada ya hapo mapambano yalizuka kati ya vikosi vya Israel na wanamgambo wa Gaza na sauti za miripuko ya mabomu zimekuwa zikirindima katika eneo zima la Gaza.Kundi la wanamgambo wa Kiislamu la Jihadi limesema mmojawapo wa makamanda wake ameuwawa na shambulio la kifaru karibu na mji ulio kusini mwa Gaza wa Khan Younis.
Mvutano wa suluhu
Vita hivyo vya siku 20 vimeuwa zaidi ya Wapalestina 1,050 wengi wao wakiwa raia wakati Israel imepoteza wanajeshi wake 43. Usitishaji wa mapigano wa saa 12 wa hapo jana uliokubaliwa na pande zote mbili kufuatia juhudi nzito za kidiplomasia za Marekani na Umoja wa Mataifa umewawezesha Wapalestina kurudi kwenye vitongoji vyao vilivyogeuzwa kuwa vifusi na kuruhusu wafanyakazi wa matibabu kufukuwa takriban maiti 150 zilizofukiwa na vifusi vya nyumba zilizoshambuliwa na Israel.
Baraza la mawaziri la Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu liliamuwa kuongeza muda wa suluhu ya kusistisha mapigano hadi usiku wa manane kwa sharti kwamba vikosi vyake viweze kuendelea kuyasaka na kuyaangamiza mahandaki yanayotumia na wanamgambo kuvuka mpaka na kuishambulia Israel.
Hamas awali ilikataa pendekezo hilo na kusema kwamba wapiganaji wake wataendeleza mapigano yake kwa kadri vikosi vya Israel vitakapoendelea kubakia Gaza.
Kundi la Hamas linalotawala Gaza ambalo limekuwa likidai Israel na Misri ziachane na hatua zao za kuifungia Gaza pamoja na kutaka kuachiliwa kwa wafungwa wanaoshikiliwa Israel imevurumisha takriban maroketi 12 katika miji ya Tel Aviv na Ashdod hapo jana lakini hakuna uharibifu au majeruhi ulioripotiwa.
Juhudi za kidiplomasia
Israel ilianzisha mashambulizi yake ya Gaza hapo Julai 8 ili kukomesha mashambulizi ya maroketi yanayofanywa na Hamas na washirika wao ambao wamekuwa katika hali mbaya chini ya vikwazo vya kiuchumi walivyowekewa na Israel na Misri kwa kuifungia Gaza pamoja na kughadhibishwa na msako wa Israel dhidi ya wafuasi wao katika eneo jirani la Ukingo wa Magharibi wanalolikalia kwa mabavu.
Hakuna hatua kubwa zilizofikiwa katika juhudi za kidiplomasia na za kimataifa kukomesha mzozo huo.
Waziri wa mambo ya nje wa Marekani John Kerry amerudi Washington wakati wa usiku baada ya kukutana mjini Paris Ufaransa na mawaziri wa mambo ya nje wa Ufaransa,Italia, Uingereza,Ujerumani,Uturuki na Qatar.
Mwandishi : Mohamed Dahman/Reuters/AP
Mhariri : Oumilkher Hamidou