1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Harakati za kuukomboa mji wa Mosul,Iraq zaingia siku ya 5

Jane Nyingi
21 Oktoba 2016

Huku majeshi ya serikali yakiendelea kuukomboa mji wa Mosul ambao umo chini ya udhibiti wa wapiganaji wa kundi la IS, wapiganaji hao wamekiri kuhusika katika mashambulizi mabaya ya kujitoa mhanga kusini mwa Iraq.

https://p.dw.com/p/2RWTz
Irak Angriff auf Mossul Peschmerga Raketenwerfer
Picha: Getty Images/AFP/S. Hamed

Hayo yanajiri huku Waziri wa Ulinzi wa Marekani, Ashton Carter, akiwasili Ankara kwa mazungumzo na viongozi wa Uturuki ambayo ni mshirika wake muhimu katika vita dhidi ya IS.  Mashambulizi hayo katika mji wa Kirkuk ambao unadhibitiwa na Wakurdi yanatazamwa kama mbinu ya IS kuwababaisha maelfu ya wanajeshi wa serikali ambao wanakaribia kuuteka mji wa Mosul. Wapiganaji hao wamesema wenzao waliovalia mikanda ya mabomu waliyavamia makao makuu ya polisi na majengo mengine ya serikali na pia kukishambulia kituo cha uzalishaji umeme kinachojengwa na kampuni moja ya Iran kaskazini mwa Iraq. Mji wa Kirkuk upo umbali wa kilomita 240 kaskazini mwa mji mkuu wa Iraq, Baghdad, na unafahamika kutokana na utajiri wake wa mafuta.

Karte Irak Kirkuk Mosul Dibis Deutsch

Mji huo ambao ni mkubwa umegawanyika kikabila na kidini, japo hivi sasa uko chini ya udhibiti wa Wakurdi. Lakini licha ya mashambulizi hayo ya kujitoa muhanga, majeshi ya serikali kwa siku ya tano mfululizo yameimarisha mashambulizi yake kwenye mji wa Mosul ambao ndio wa pili kwa ukubwa nchini Iraq, ili kuuondoa mikononi mwa mwa IS.

Majeshi ya Iraq yapongezwa

Wanasiasa na viongozi wa kijeshi wamewapongeza wanajeshi kutokana na jinsi walivyoweza kuwakabili haraka wapiganaji hao kinyume na ilivyotazamiwa, japo nao wameyajibu mashambulizi hayo kwa kusababisha mauaji mabaya ya majeshi ya Iraq. Wakristo hasa waliohama mji huo wa Mosul baada ya kuwa chini wa udhibiti wa IS wamekuwa wakifuatilia matukio kupitia radio na televisheni "Mungu akipenda tutarejea nyumbani. Tumeteseka vya kutosha, inauma. Tulihama na kuyaacha makaazi yetu. Hali ni mbaya" anasema mmoja wa wakaazi

Irak Flüchtlinge in Dohuk 13.08.2014
Wakristo waliolazimika kuhama mji wa MosulPicha: picture-alliance/dpa

Naye. Waziri wa Ulinzi wa Marekani, Ashton Carter, hii leo anafanya mazungumzo na Rais Tayyip Edogan wa Uturuki, Waziri Mkuu Binali Yildirim na Waziri wa Ulinzi Fikri Isik kuhusu mashmabulizi hayo yanayoendelea nchini Iraq. Marekani ina wasiwasi kuhusu tahuruki iliyopo kati ya Uturuki na Iraq, huku majeshi ya serikali yakitazamiwa kuuteka mji wa Mosul kutoka kwa IS.

Uturuki ambayo ina wasiwasi kuwa mashambulizi hayo ya Mosul huenda yakaongeza ushawishi wa wapiganaji wa Kikurdi ambao inawapinga, imesema haiwezi kusalia pembeni wakati mashambulizi hayo yakiendelea, japo Baghdad imepinga vikali kuhusika kwa majeshi ya Uturuki katika mashambulizi hayo.Marekani inaitaka Uturuki kujizuia na operesheni za kijeshi nchini Iraq, kwa kuhofia kuwa majibizano hayo kati ya Uturuki na Iraq huenda yakavuruga makubaliano ya kuwaondoa wapiganaji na makundi ya siasa kali katika mji wa Mosul.

 

Mwandishi: Jane Nyingi AFPE/AP

Mhariri: Mohammed Khelef