Harris atokea kwa mara ya kwanza kwenye kampeni
13 Agosti 2020Mgombea mwenza wa urais kupitia chama cha Democrats nchini Marekani Kamala Harris ametokea kwa mara ya kwanza kwenye kampeni za urais za Joe Biden hapo jana, kwa kumkosoa rais Donald Trump kwa kushindwa kulikabili vilivyo janga la virusi vya corona.
Siku moja baada ya Biden kumteua, Harris na Biden wameshikishana historia ya mahusiano baina ya familia zao na ajenda kuelekea ikulu ya White House.
Harris, seneta wa California mara moja alianza kumshambulia Trump akisema amewaingiza hatarini Wamarekani kwa kushindwa kulichukulia kwa umakini janga hilo na kuitumbukiza Marekani kwenye mzozo wa kiuchumi, katika wakati ambapo inapambana na kukosekana kwa usawa wa rangi na kijamii.
Alisema, "Huu ni wakati wa matokeo halisi kwa Marekani. Kila kitu kilicho muhimu kwetu, uchumi wetu, afya, watoto wetu na aina ya taifa tunalosihi, kila kitu kipo kwenye mstari. Tuko katika mzozo mbaya kabisa wa kiafya wa karne. Rais ameshindwa kushughulikia janga hili na kututumbukiza kwenye mzozo mbaya kabisa wa uchumi kuwahi kutokea tangu mdororo mkubwa kabisa wa uchumi."
Alipomtambulisha, Biden alisema amefanya chaguo linalostahili, kwa Harris kujiunga na kampeni zake, akisema ameonyesha utayari tangu siku ya kwanza na kwa pamoja wako tayari kulijenga upya taifa hilo.
"Serikali ya Joe Biden na Kamala Harris itakuwa na mkakati thabiti wa kukabiliana na COVID-19 utakaobadilisha hali ya mambo. Uvaaji wa barakoa, kuongeza upimaji na kuziwezesha serikali za majimbo ili kufungua shule na biashara kwa usalama. Tunaweza. Tunachohitaji ni rais na makamu walio tayari kuongoza na kuwajibika", alisema Biden.
Kutokea kwao kwa pamoja kunakuja siku chache kabla Biden hajakubali rasmi kuwa mgombea wa urais wa chama cha Democrat katika kongamano la chama wiki ijayo, ambalo kwa kiasi kikubwa litafanyika kwa njia ya mtandao kutokana na janga la virusi vya corona.
Harris awataka Wamarekani kutumia fursa waliyonayo kufanya maamuzi.
Harris alitangazwa na Biden siku ya Jumanne baada ya mchakato wa uchaguzi. Budeni, aliyewahi kuwa makamu wa rais atakuwa rais wa kwanza mwenye umri mkubwa zaidi iwapo atashinda, hali inayoibua minong'ono kwamba hatagombea awamu ya pili mwaka 2024.
Harris, mwanamke wa kwanza mweusi na wa kwanza mwenye asili mchanganyiko wa Marekani na Asia anayegombea wadhifa huo wa juu wa urais, ni binti wa muhamiaji, mama yake akitokea India na baba yake, Jamaica.
Amewataka Wamarekani kuikataa serikali ya Trump iliyoshindwa. Amesema katika siku 83 zilizosalia, wana fursa ya kuamua kuhusu mustakabali mzuri wa taifa hilo. Harris amesisitiza, yeye na Biden watalirudisha taifa hili kwenye hali nzuri.
Katika hatua nyingine, Biden amekusanya kiasi cha dola bilioni 26 ambazo ni mara mbili ya kiwango cha awali cha siku moja. Biden amekusanya fedha hizo, katika kipindi cha masaa 24 baada ya kumtaja Harris kuwa mgombea mwenza, hali inayoashiria kukubalika kwa Harris miongoni mwa Wademocrats.
Mashirika: RTRE/DPAE