Harris na Trump warushiana vijembe kwenye kampeni Wisconsin
31 Oktoba 2024Zikiwa zimebaki siku sita kuelekea uchaguzi wa Marekani, mgombea wa chama cha Democratic, Kamala Harrris katika hotuba yake akiwa kwenye Chuo Kikuu cha Wisconsin mjini Madison, Harris amesema ni wakati wa uongozi wa kizazi kipya kuingia madarakani nchini humo.
Mgombea huyo wa Democratic anayeongoza kwa kiasi kidogo katika kura ya maoni dhidi ya Trump katika jimbo hilo ameongeza kuwa wapiga kura katika uchaguzi huo wana nafasi ya kufunga ukurasa wa muongo mmoja wa Donald Trump anayejaribu kuwagawanya na kuwafanya waogopane. Amewaeleza wafuasi wake kwamba ni wakati wa kizazi kipya kuiongoza Marekani na yuko tayari kuwapa aina hiyo ya uongozi kama raisi ajaye wa Marekani.
Harris amewaahidi pia wafuasi wake kuwa iwapo atachaguliwa atafanya juhudi za kutafuta suluhisho kwa matatizo yanayowakabili na kwamba hahitaji kupata alama za kisiasa bali anataka maendeleo. Mgombea huyo wa Democratic amekuwa akitumia muda mwingi wa kampeni zake kuwafikia waliowahi kuwa wafuasi wa Trump na wasiokubaliana na siasa zake. Amekuwa pia akiwatambulisha wafuasi hao wa zamani wa Trump akijinadi kuwa anataka kuwashirikisha Warepublican katika Baraza lake la Mawaziri kama atachaguliwa.
Trump atumia gari la kubeba taka kwenye kampeni
Kwa upande wake mgombea wa Republican na Rais wa zamani Donald Trump katika jimbo hilo hilo, alionekana kwenye kampeni akiwa amepanda kwenye gari la taka hatua inayotafsiriwa kuwa ni jibu kwa kauli ya Rais Joe Biden iliyotolewa hivi karibuni iliyoashiria kuwaita wafuasi wa Trump kuwa sawa na "takataka".
Akizungumza katika mkutano huo wa kampeni katika eneo la Green Bay, Trump amefafanua kuwa, alichokisema Biden kinaakisi namna wawili hao wanavyowachukulia wafuasi wake. Ameeleza kwamba maoni ya Rais Biden ni matokeo ya moja kwa moja ya uamuzi wa mpinzani wake Kamala Harris wa kumwona yeyote asiyempigia kura kuwa ni shetani na si binadamu kamili.
Katika kampeni hiyo Trump ameongeza kuwa Biden na makamu wake wamekuwa wanaichukulia nchi nzima kuwa takataka kwa kufungua mipaka na kuruhusu mfumuko wa bei na yanayoendelea Urusi na Ukraine. Trump amesema, migogoro yote aliyoitaja isingetokea kama Marekani ingelikuwa na rais tofauti.