Harusi ya kifalme ya Harry na Markle Uingereza
19 Mei 2018Mamilioni ya watazamaji katika televisheni duniani kote wanatarajiwa kushuhudia wakati wageni wakianza kuwasili majira ya saa tatu unusu saa za Uingereza, ambapo ndugu katika familia ya kifalme watafuata baada ya saa 5.
Mamia ya hafla za kibiashara na kijamii zimetayarishwa kote nchini Uingereza kuadhimisha sherehe hiyo ya harusi.
Harry mwenye umri wa miaka 33, na Markle mwenye umri wa miaka 36, walilala katika hoteli tofauti karibu na Windsor usiku wa Ijumaa (18.05.2018).
Harry alijumuika na kaka yake na ambaye ni msaidizi wake wa karibu katika harusi hiyo, mwanamfalme William , mwenye umri wa miaka 35, wakati mama yake Markle mwenye umri wa miaka 62, Doria Ragland, akiongozana nae.
Kiasi ya wageni 600 wanatarajiwa kuhudhuria katika kanisa itakapofanyika harusi hiyo na hafla ya baada ya harusi ambayo itaongozwa na Malkia Elizabeth wa pili katika kasri. Baba yake Harry, Mwanamfalme Charles , anaongoza hafla ya jioni kwa wageni maalum 200 katika nyumba ya karibu na hapo ya Frogmore.
Harusi ya kufana
Tukio hilo la harusi litakalochukua muda wa saa moja litafuatiwa na msafara wa dakika 20 nje ya kasri katika gari la kukokotwa na farasi, kabla ya hafla hiyo itakayoongozwa na malkia.
Markle alitangaza siku ya Alhamis kwamba baba yake hatahudhuria harusi hiyo. Thomas Markle, mwenye umri wa miaka 73, alifanyiwa upasuaji wa moyo siku ya Jumatano.
Makao makuu ya kifalme yamesema Charles atatembea na Markle katika ukumbi wa kanisa ili kumkabidhi mwanawe kwa ajili ya harusi hiyo. Harry na Markle wamewakaribisha mamia ya watu kushuhudia sherehe hizo katika viwanja vya kasri la kifalme, wakati mamia kwa maelfu ya watu wanaosherehekea harusi hiyo wakijipanga katika njia itakamopita gari ya kukokotwa na farasi.
Polisi imepiga marufuku kurusha maua na mapambo wakati wa msafara huo , wakielezea kuhusu wasi wasi wa usalama.
Uingereza imekuwa ikivutia dunia kwa harusi za kifalme, matukio ya sherehe za kuvutia na haiba ambayo inasababisha mvuto kwa familia ya kifalme.
Mwandishi: Sekione Kitojo / dpae
Mhariri: Daniel Gakuba