Hatua ya makundi yakaribia mwisho
21 Juni 2021Hatua ya mechi za mkundi ya michuano ya kandanda Ulaya inakaribia ukingoni, timu 16 zitajikatia tiketi zao katika duru ijayo. Mashindano hayo ya Euero 2020 yenye timu 24 taratibu inageuka sasa kuwa mashindano ya timu 16..ni timu mbili za kwanza kwenye kila kundi pamoja na timu nne bora za nafasi ya tatu ndizo zitaingia hatua ya mtoano. Hii ina maana kuna na kizaazaa katika mechi hizi za mwisho za makundi. Kama tu ilivyo katika mashindano mengi makubwa, baadhi ya watakaonusurika katika hatua ya makundi yatakuwa majina ya kawaida na yanayotarajiwa, lakini mengine yatakuwa ya mshangao. Italia inaonekana kuwa timu iliyokamilika kabisa baada ya kupata ushindi wake wat atu jana kwa kuifunga Wales 1 – 0. Kocha Roberto Mancini anasema mashindano sasa ndio yanaanza akimaanisha hatua ya mtoano "Nilifurahishwa sana na ukweli kwamba tulibadilisha wachezaji wanane na timu bado ikacheza vizuri sana. tulistahili kufunga mabao zaidi, lakini haikuwa rahisi kwa sababu walijilinda vizuri sana. Hiki ndicho nilichofurahishwa sana nacho kwa timu yangu. vijana walijituma sana." Amesema Mancini
Katika muda mfupi ujao, Denmark inaialika Urusi mjini Copenhagen, ikiwa bado na fursa ya kutinga 16 za mwisho licha ya kupoteza mechi zake mbili za kwanza.
Denmark inaweza kumaliza katika nafasi mbili za kwanza za Kundi B kama itaifunga Urusi nayo Ubelgiji ambayo tayari imefuzu, ishinde dhidi ya Finland baadaye leo.
Urusi itahitaji pointi moja tu ili kufuzu katika nafasi ya pili kama Ubelgiji itashinda. Katika mechi nyingine, Austria itafuzu kutoka Kundi C kwa ushindi mjini Bucharest dhidi ya Ukraine, ambao watafuzu kama wataepuka kichapo.
Mechi nyingine ya leo katika Kundi C isiyo na maana ni kati ya Uholanzi, ambao wamejihakikishia nafasi ya kwanza, na Macedonia Kaskazini ambao tayari wamefungashwa vilago.
Wales walisherehekea kutinga 16 za mwisho licha ya kupoteza 1 – 0 kwa Italia na kumaliza wa pili katika Kundi A. Uswisi watasubiri kujua kama watajiunga nao baada ya kuwapiga Uturuki 3 - 1.
Hata hivyo kibarua kikali kitakuwa kesho katika Kundi F ambalo lipo wazi kabisa, likiwa na mabingwa watetezi wa Ulaya Ureno, mabingwa watetezi wa dunia Ufaransa, Ujerumani na Hungary. Ujerumani itavaana na Hungary wakati Ufaransa ikikamatana na Ureno.
AFP/AP/Reuters