Hillary Clinton aihitimisha ziara ya Tanzania
13 Juni 2011Bi Clinton, aliyewasili nchini Tanzania mwishoni mwa juma akitokea Lusaka, Zambia, amekuwa na majadiliano ya faragha na Rais Jakaya Kikwete na baadaye kukutana na waandishi wa habari ambako wote kwa pamoja wamezungumzia mkwamo wa kisiasa unavyojiri huko Zimbabwe na machafuko yanayoendelea sasa katika jimbo la Abyei, nchini Sudan.
Usuhuba mzuri
Kabla ya kufikia hoja hiyo kwanza walijadiliana siasa za nchi mbili-yaani Tanzania na Marekani- ambako wakaeleza kuwa mataifa hayo yanaendelea kudumisha mahusiano yao na kuahidi kuongeza maingiliano zaidi kwenye sekta za uchumi na biashara.Rais Kikwete aliisifu Marekani namna inavyoendelea kutoa mchango kusaidia sekta za afya, elimu na maeneo mengine iikwemo ukuzaji uchumi na maendeleo
Amedai kuwa mashirikiano hayo yamesaidia pakubwa kusukuma mbeleo ustawi wa maisha na ukuzaji uchumi. Eneo alilolitaja kupata mafanikio makubwa ni juu ya mapambano ya ugonjwa wa Malaria ambako amesema hali ya ugonjwa huo imedhibitiwa vyakutosha.
Uchumi na Biashara
Lakini pia viongozi hao wamejadiliana juu ya masuala ya uchumi na biashara. Katika miaka ya hivi karibuni hali ya ufanyaji biashara ya moja kwa moja baina ya mataifa hayo mawili imekuwa katika kiwango cha kurishisha, na wataalamu wa masuala ya uchumi wanaona kuwa ongezeko hilo linatazamiwa kuendelea kukaa zaidi
katika kipindi kijacho.
Kwa mwaka jana pekee, Marekani ilisafirisha bidhaa nchini Tanzania zinazofikia thamani ya dola milioni 164, wakati Tanzania ilifanikiwa kuvuna kiasa cha dola milioni 43 kutokana na bidhaa zake iliyosafirisha katika soko la Marekani.
Mchango wa kisiasa
Na katika siasa za kimataifa, Waziri huyu wa mambo ya nje amezihimiza nchi wanachama wa Jumuiya ya maendeleo kusini mwa Africa -SADC- kuongeza juhudi ili kutatua mkwamo wa kisiasa unaoikabili serikali ya umoja wa kitaifa ya Zimbabwe.
Alipogeukia hali ya mambo huko Sudan hasa katika jimbo la Abyei, ambako serikali ya Al Bashiri imepeleka vikosi vyake, Bi Clinton ametaka Khartoum kutambua kuwa inawajibu wa kusimamia mchakato wa ufikiaji amani kwa kufuata maridhiano yaliyofikia hapo kabla nataka iviondoshe vikosi vyake kwenye eneo hilo.
Bi Clinton kwa hivi sasa ameelekea nchini Ethiopia ambako anatazamiwa kujadiliana na mwenyeji wake kuhusu siasa za Pembe ya Afrika.
Mwandishi: Njogopa, George
Mhariri: Othman,Miraji