Hong Kong: Maelfu waandamana mitaani kudai uhuru kamili
2 Novemba 2019Maandamano mapya yalianza mjini Hong Kong Jumamosi (02.11.2019) wakati kukiwa na wasiwasi kwamba China inapanga kuzidisha udhibiti wake katika mji huo. Kiasi ya waandamanaji 3,000 walikusanyika katika viwanja vya Victoria Park, eneo ambalo limekuwa kitovu cha maandamano.
Polisi walitumia gesi ya kutoa machozi kutawanya maandamano ambayo mamlaka zinasema hayakuwa na kibali cha kufanyika. "Serikali nzima inadhibitiwa na serikali kuu hivi sasa, kwahiyo tumekuja hapa kuandamana ili kulinda uhuru wetu tunaostahili", alisema kijana mmoja wa miaka 17 alipozungumza na AFP.
China ilitangaza siku ya Ijumaa kwamba haitovumilia upinzani wowote wa kuingilia mfumo wa serikali wa Hong Kong. Pia inapanga kuongeza elimu ya uzalendo mjini Hong Kong.
Baadhi ya waandamanaji walimiminika mitaani kwenye eneo la maduka la Causeway Bay. Polisi wa kupambana na ghasia walikuwepo eneo hilo na kufanya upekuzi huku wakionya kwamba mkusanyiko wowote si halali. Hata hivyo waandamanaji wengi walikaidi marufuku ya serikali ya kuficha nyuso zao na vitambaa maalumu. Wengi walivaa vifaa maalum vya kujikinga na gesi.
Wito wa Dharura
Mwanaharakati wa kudai demokrasia Joshua Wong aliwatolea wito watu 100,000 kushiriki maandamano ya Jumamosi ya kupinga serikali. Aliandika kupitia Twitter kwamba "Utekelezaji wa uhuru wa mkusanyiko umezidi kuwa mgumu kwasababu polisi wa Hong Kong wamekuwa wakitumia nguvu katika miezi ya hivi karibuni. Ndio! hatukati tamaa juu ya haki yetu ya kikatiba".
Mwanaharakati huyo ameyaelezea maandamano mapya kama "wito wa dharura" wa ongezeko la kudai uhuru kamili. Waandamanaji wengi walibeba bendera za Uingereza au zile za kikoloni kwa kuzingatia ahadi iliyotolewa na Uingereza mwaka 1997 wakati wa makabidhiano.
Maandamano ya Hong Kong yalianza mwezi Juni mwaka huu kupinga pendekezo la kuwaruhusu wahalifu kushitakiwa China bara. Katika miezi iliyofuata, waandamanaji walianza kudai uchaguzi wa moja kwa moja kwa ajili ya viongozi wa Hong Kong . Wiki hii ni ya 22 ya maandamano yasiyomalizika mjini Hong Kong huku mji huo ukitaraji kufanya uchaguzi wa halmashauri ya wilaya mwezi ujao.
dw/dpa