HRW: mateso ya wafungwa wa Uturuki yakiuka haki za binaadamu
25 Oktoba 2016Shirika hilo la kimataifa la kutetea haki za binaadamu lilikuwa likichunguza madai ya mateso dhidi ya watu waliowekwa kizuizini baada ya jaribio la mapinduzi yaliyozimwa mwezi Julai. Serikali ya Uturuki imewakamata watu wapatao 35,000 wanaoshukiwa kuhusika na kupanga njama za mapinduzi hayo.
Wengi wa wafungwa hao wamekamatwa kwa madai ya kuwa na mahusiano na kiongozi wa kidini, Fethullah Gulen, ambaye anashutumiwa na serikali ya Uturuki kwa kupanga mapinduzi hayo.
Wengine wamewekwa kizuizini kwa madai ya kukisaidia Chama cha Wafanyakazi wa Kikurdi (PKK), kilichopigwa marufuku na ambacho kimekuwa kikipambana kwa muda mrefu na wanajeshi wa Uturuki katika eneo lenye Wakurdi wengi kusini mashariki mwa nchi hiyo.
Lakini ripoti hiyo inasema hali ya hatari iliyotangazwa nchini humo, haiiruhusu serikali kutozingatia haki za binaadamu. Aidha ripoti hiyo inatoa maelezo juu ya visa 13 vya madai ya unyanyasaji yanayofanywa na maafisa wa Uturuki dhidi ya wafungwa, ikiwa ni pamoja na kupigwa, kuteswa na unyanyasaji wa kingono.
Shirika hilo lilichunguza madai yaliyoripotiwa katika mji mkuu wa Ankara, Istanbul, Urfa pamoja na Antalya.
"Nitambaka mzazi wako mbele yako"
Shirika la Human Rights Watch lilizungumza na mwanasheria wa mmoja wa wafungwa hao ambaye alimsimulia mateso yaliyomfika.
"Walinivua nguo zangu huku wakizichana, walinitisha huku wakiziminya sehemu zangu za siri na kunipiga vibaya sana," amenukuliwa na wakili wake akisema. Mmoja wa maafisa alimwambia "nimemleta mama yako hapa, ukikataa kuzungumza nitambaka mbele yako."
Katika kisa kingine, mke wa mfungwa mmoja miongoni mwa waliokamatwa katika mji wa Antalya anasema ilibidi mumewe akatwe sehemu ya utumbo wake mdogo kwa sababu aliumizwa vibaya alipokuwa akiteswa.
Wanaharakati wa shirika la Human Rights Watch walizungumza na wanasheria kadhaa pamoja na watuhumiwa waliosema kwamba mamlaka za Uturuki zilitumia mateso kuwashinikiza kutoa ushahidi.
Miongoni mwa njia zenye utata zinazotumiwa kuwadhibiti wafungwa na zinazokiuka haki zao ni kuongezwa kwa idadi ya siku kutoka 4 hadi 30 ambapo mtuhumiwa anawekwa kizuizini baada ya kukamatwa kabla ya kumfikisha au kupeleka shitaka lake mahakamani. Pamoja na hayo mtuhumiwa anaweza kucheleweshewa haki yake ya kukutana na mwanasheria kwa zaidi ya siku tano.
Shirika la Human Rights Watch limeitolea wito serikali ya Uturuki kufuta mara moja amri za mateso zinazotumika katika kipindi cha hali ya dharura, na kusema kuwa zinakiuka sheria za kimataifa.
Mwandishi: Yusra Buwayhid/dpae
Mhariri: Caro Robi